Korea yaisaida AfDB kuchochea maendeleo ya uchumi Afrika

Naibu katibu mkuu Fedha na Mipango, Amina Shaaban akisalimiana na Rais waAfDB, Dk Akinwumi Adesina kwenye mkutano wa sita wa jukwaa la ushirikiano kati ya Korea Kusini na Afrika jijini Busan, Korea Kusini. Na Mpigapicha maalumu

Dar es Salaam. Jamhuri ya Korea Kusini imesaini mkataba wa kuipa Benki ya Maendelea Afrika (AfDB) Dola 5 bilioni za Marekani (zaidi ya Sh11.25 trilioni), ili kufanikisha miradi mbalimbali ya maendeleo.

Fedha hizo zitatolewa ndani ya miaka miwili kutoka mashirika tofauti ya Taifa hilo. Rais wa AfDB, Dk Akinwumi Adesina na makamu waziri mkuu wa Korea, Dong Yeon Kim walisaini mikataba mitatu kufanikisha matumizi ya fedha hizo.

Mikataba hiyo ilihusisha ule wa ushirikiano wa kiuchumi kati ya Korea na Afrika (Koafec), utakaotoa Dola 600 za Marekani kwa ajili ya miradi ya umeme na wa kuimarisha ubunifu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama).

“Afrika inahitaji kujenga na tutajenga uhusiano mpana wa maendeleo. Tunahitaji kuwa na ubia imara wa uwekezaji na bara la Asia,” alisema Dk Adesina.

Makubaliano hayo yameafikiwa jijini Busan, Korea Kusini ambako AfDB inafanya mkutano wake wa 53 wa mwaka ambao unawashirikisha mawaziri wa fedha Afrika wanaounda bodi ya magavana wa benki hiyo.

AfDB imewataka magavana wa Afrika kuzisaidia nchi zao kutatua changamoto za kiuchumi na kuhamasisha maendeleo endelevu, ili kuendana na mapinduzi makubwa yanayotokea duniani kwa kuhamasisha ukuaji wa viwanda.

Rai hiyo imetolewa na Rais wa Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB), Dk Akinumwi Adesina wakati wa mkutano wa sita wa jukwaa la ushirikiano kati ya Jamhuri ya Korea Kusini na Afrika uliojadili namna bora ya kuchochea ukuaji wa viwanda barani Afrika.

“Afrika inahitaji mapinduzi ya kiuchumi kwa kuwekeza kwenye viwanda na miundombinu kusaidia kukuza uchumi wa nchi kwa kasi na kuleta maendeleo yenye tija,” alisema Dk Adesina.

Kwa upande wake, makamu waziri mkuu wa Kora Kusini alisema Afrika inahitaji ushirikiano wenye manufaa na wahisani likiwamo Taifa lake, ili kuharakisha maendeleo ya kiuchumi kwa kubadilishana uzoefu na kubaini fursa za ukuaji uchumi utakaochochea ushirikiano huo.

“Afrika ina fursa nyingi za kukuza uchumi, ina rasilimali za kutosha katika sekta zote muhimu za maendeleo ikiwamo madini, kilimo, mifugo na uvuvi,” alisema Kim.