TMRC yapewa kibali kuuza dhamana ya Sh120 bilioni kujenga nyumba

Ofisa mtendaji mkuu wa kampuni ya Orbit Securities, Juventus Simon akipokea hati ya matarajio ya mauzo ya dhamana ya TMRC ya Sh120 bilioni baada ya kuidhinishwa na Mamlaka ya Masoko na Mitaji (CMSA) kutoka kwa mkurugenzi wa utafiti, sera na mipango wa mamlaka hiyo, Alfred Mkombo. Wanaoshuhudia, kushoto ni meneja mawasiliano wa CMSA, Charles Shirima na katikati mkurugenzi wa fedha TMRC, Oswald Urassa. Na Mpigapicha Maalumu

Muktasari:

Hatua hiyo kuiongezea mtaji kampuni ili iwewe kupanua shughuli zake

Dar es Salaam. Kampuni ya Mikopo ya Nyumba Tanzania (TMRC), imepata kibali cha kuuza dhamana yake ya Sh120 bilioni itakayoiva ndani ya miaka mitano.

Ofisa mtendaji mkuu wa TMRC, Oscar Mgaya alisema tayari Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) na Soko la Hisa Dar es Salaam (DSE) zimeidhinisha uuzaji wa dhamana hiyo.

“Mamlaka zote zimetupa kibali cha kuuza dhamana yetu. Tutaiuza muda wowote kuanzia sasa,” alisema Mgaya.

Dhamana ya kampuni (corporate bond) huuzwa kupata mtaji utakaofanikiwa utekelezaji wa mipango mbalimbali iliyojiwekea kampuni husika kama vile operesheni zilizopo, ununuzi wa kampuni nyingine au kupanua operesheni.

Mgaya alisema TMRC inauza dhamana hiyo kufanikisha operesheni zake za utoaji wa mikopo ya nyumba kwa benki za biashara na taasisi za fedha nchini.

“Tangu kuanzishwa kwake, TMRC, ilielezwa kwamba itatengeneza mtaji kutoka kwenye masoko ya hisa na dhamana. Lilikuwa ni suala la muda tu, sasa ni wakati mwafaka wa kulitumia soko,” alisema Mgaya.

Akizungumzia utekelezaji wa suala hilo, msemaji wa CMSA, Charles Shirima alithibitisha kuridhiwa kwa uuzwaji wa dhamana ya kampuni hiyo akisema imekidhi vigezo vyote muhimu vinavyopaswa kuzingatiwa.

“Wiki iliyopita bodi ya ilitoa kibali cha mauzo ya dhamana ya TMRC. Watakapokuwa tayari watakamilisha utaratibu uliobaki na kuifikisha sokoni,” alisema Shirima.

Tangu ilipoanzishwa mwishoni mwa miaka ya 2000 mpaka sasa, TMRC ina wanachama 31 wanaotoa mikopo ya nyumba huku benki tano zikiwa na asilimia kubwa zaidi.

Kati ya benki hizo zinazohudumia Watanzania wengi zaidi ni Stanbic yenye asilimia 18, Bank M asilimia 16 na CRDB asilimia 11. Nyingine ni Azania yenye asilimia nane na CBA yenye asilimia saba.

Ndani ya muongo mmoja uliopita, benki hiyo imeongeza idadi kubwa ya benki za biashara na taasisi za fedha zinazotoa mikopo kupunguza uhaba wa nyumba milioni tatu uliopo nchini.

Takwimu zinaonyesha, kila mwaka, maeneo ya mjini yanahitaji nyumba mpya 200,000 kutokana na ongezeko la watu lakini zinazojengwa ni 15,000 pekee.