Tamu, chungu ya bajeti Dodoma

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango

Muktasari:

Ni bajeti ambayo wananchi wana matarajio ya kuona namna gani itawaletea maendeleo

Dodoma. Tamu na chungu za Bajeti Kuu ya Serikali ya mwaka 2018/19 itajulikana leo wakati Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango atakapoiwasilisha bungeni.

Waziri Mpango ataisoma bajeti hiyo bungeni jijini Dodoma ikiwa ni bajeti ya tatu ya utawala wa awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli tangu ulipoingia madarakani Novemba 5, 2015 ikitanguliwa na ya mwaka 2016/17 iliyokuwa ya Sh29.5 trilioni na inayoishia ya 2017/18 ya Sh31.7 trilioni

Ni bajeti ambayo wananchi wana matarajio ya kuona namna gani itawaletea maendeleo huku wabunge wakitoa mtazamo wao juu ya bajeti hiyo wakisema inahitaji kuangazia maisha ya wananchi moja kwa moja na upunguzaji wa ada, tozo na kodi mbalimbali.

Kuwasilishwa kwa bajeti hiyo ni baada ya kuhitimishwa kwa bajeti za wizara zilizoanza kujadiliwa Aprili 3 hadi Juni 5 ambapo ilishuhudiwa mvutano wa hapa na pale hasa kutokana na fedha zilizotengwa kutopelekwa kama zilivyopitishwa na Bunge.

Jana, Mwananchi ilizungumza na baadhi ya wabunge juu ya kile wanachotarajia kukiona katika bajeti hiyo na wengi walisema inatakiwa iwe ya kujibu mahitaji ya wananchi.

Mbunge wa Welezo (CCM), Saada Mkuya alisema bajeti anayotarajia ni ile itakayokuwa rafiki na miundombinu ya wananchi wa hali ya chini kwa ajili ya maendeleo yao.

“Sina maana miradi mikubwa isifanyike hapana, ila ninataka bajeti ambayo wakati tunajenga miundombinu mikubwa basi tuangalie na hali ya wananchi wetu wa chini, mfano bajeti ilenge kuboresha huduma za maji, vituo vya afya, umeme na barabara vijijini,” alisema

Mkuya aliyewahi kuwa Waziri wa Fedha katika utawala uliopita wa Rais mstaafu Jakaya Kikwete alisema bila ya kufanya hivyo, kuna uwezekano mkubwa kuwepo na bajeti nzuri lakini wananchi wakashindwa kuitafsiri kwa sababu maendeleo yao yanakuja kwa vitu vinavyowafikia moja kwa moja.

Alitolea mfano wa maji kuwa yakichimbwa leo na leo wanaanza kutumia ikilinganisha na reli ikijengwa leo manufaa yake yataonekana baada ya muda mrefu.

Waziri kivuli wa Fedha na Mipango, Halima Mdee alisema, “changamoto kubwa, hatuko wakweli juu ya uwezo wetu wa kukusanya mapato yetu ya ndani jambo linalokwamisha utekelezaji wa bajeti nzima.”

“Serikali inasema tuna uwezo wa kukusanya Sh17 trilioni lakini ni ukweli usiopingika, kwa miaka kumi iliyopita, toka Jakaya (Kikwete)uwezo wetu wa kukusanya ni Sh12 trilioni, ukichanganya na maduhuli na mapato ya halmashauri, makusanyo ya TRA hayazidi Sh14 trilioni,” aliongeza Mdee ambaye pia ni Mbunge wa Kawe (Chadema).

Mdee alisema, “tunahitaji kujenga mazingira rafiki kwa walipaji kodi na si mtu akianza biashara tu unadai kodi ambazo ni kali na lazima tuwape muda wawekezaji wanaokuwa kuwekeza kipindi cha mpito si mtu hajaanza biashara unadai kodi, tutawakimbiza.”

Mbunge wa Mlalo (CCM), Rashid Shangazi alisema, “bajeti hii nataka ije kutoa ufafanuzi zaidi wa Tanzania ya viwanda.”

“Tuwe na uzalishaji mwingi wa mazao ya kilimo ili viwanda vyetu vitumie malighafi za kilimo lakini suala la mifugo, tusiwe na mifugo inayozurura nchi nzima, hivyo bajeti inapaswa kuangazia eneo hili hasa kuwa na viwanda vya nyama.”

Shangazi alisema hata mazao yanayotokana na samaki bado hatujaweza kuyavuna, “haiwezekani kutoka Tanga hadi Msimbati (Mtwara) hakuna kiwanda hata kimoja cha samaki, kwa hiyo tunapaswa kuwa na viwanda vya samaki na nyama vya kutosha.”

Mbunge wa Vunjo (NCCR-Mageuzi), James Mbatia alisema, “kwa mtazamo wangu, ili uweze kupata matumaini mazuri katika slogani ya viwanda, utu wa binadamu upewe kipaumbele. Lazima kurudisha matumaini ya Watanzania kuishi. Wengi wanakata tama.”

“Mimi niko vijijini, hali ya maisha ni ngumu sana, tunataka kuona bajeti ya kukuza utu, kutoa huduma za msingi za binadamu ili apate milo mitatu, maji safi na salama, afya na kufurahia uhuru wao,” aliongeza.

Mbatia alisema, “tunahitaji kuona bajeti yenye kuonyesha maendeleo ya watu na si vitu. Ukiangalia kwa kiasi kikubwa, miundombinu ilivyoharibika, shule, walimu na wananchi wanalalamika kwa kukosa matumaini, bajeti ikirejesha matumaini, hata viwanda vitajengeka.”

Alisema bajeti iwekeze na kuwekeza katika huduma za msingi, “ikiwamo suala la kodi, si kila sehemu hadi mama lishe, machinga. Vyanzo vya mapato vya kodi vya halmashauri virudishwe huko kwani huko ndiko wananchi waliko, lakini halmashauri zikiwa hoi bin taabani usitegemee maendeleo.”

Mbatia ambaye pia ni mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi alisema bajeti ije na mwanga wa matumaini kwa walipa kodi, “iwe bajeti rafiki kwa wafanyabiashara wazawa ili mzunguko wa fedha uwe humu humu nchini. Lakini wafanyabishara wazawa wakikata tamaa na kufunga biashara zao wanakwenda nje, huwezi kupata kodi.”

Mbunge wa Rufiji (CCM), Mohamed Mchengerwa alisema, “hii ni bajeti ya tatu ya Serikali ya awamu ya tatu ilipoingia madarakani (Novemba 5, 2015). Bajeti ya kwanza ilikuwa ya kubana matumizi na fedha zilielekezwa kwenye miradi ya maendeleo.”

Mchengerwa alisema, “bajeti hii itakayosomwa kesho (leo) ni ya kati kwenda mwaka 2019 na bajeti ya mwisho inayotoa taswira ya kile kilichoahidiwa na Rais (John Magufuli) na Ilani ya CCM (ya mwaka 2015/2020).”

“Serikali inapaswa kutekeleza yale iliyoahidi kwa wananchi hasa zile ahadi za Rais na ilani ya CCM. Kama vile kuweka mazingira mazuri ya miundombinu ya umeme hasa ile hoja ya umeme wa Stigler’s Gorge jimboni kwetu Rufiji,” alisema.

Mchengerwa alisema, “natarajia kuona ahadi ya Sh50 milioni inatekelezwa, utashuhudia katika mjadala wa wizara ya fedha, iliibuka hili la Sh50 milioni kila kijiji na wananchi wanataka kuona linatekelezwa.”

Mbunge wa Kalenga (CCM), William Mgimwa alisema, “natarajia itakuwa bajeti nzuri kutokana na kile kilichojionyesha katika bajeti za kisekta.”

Mgimwa aliongeza, “ninachokiona mimi, bajeti iwe ya kuwalenga wananchi moja kwa moja.”

Mbunge wa Mafinga (CCM), Cosato Chumi alisema kwake yeye bajeti nzuri ni ile itakayozingatia mambo makuu mawili na anaweza kuiunga mkono na kuipongeza Serikali kwa hayo.

Alitaja mambo hayo ni bajeti inayoweza kumaliza miradi viporo na hasa ile ambayo ilianzishwa na wananchi lakini Serikali inashindwa kupeleka fedha kumalizia miradi hiyo na hakuna majibu.

“Kwa mfano, wilaya ya Mafinga tuna miradi inayohitaji Sh1 bilioni lakini Serikali imeshindwa kupeleka fedha kwa ajili ya kumalizia miradi hiyo, kwa hiyo kama itakuja kwa mtazamo huo bado hatutaeleweka,” alisema Chumi.

Kingine ni bajeti ya kujenga mazingira rafiki na wafanyabiashara kwani tunakoelekea siyo kuzuri kwa sasa maana kufanyabiashara Tanzania imekuwa ni kama kutupa mitaji kutokana na utitiri wa tozo zake.

Mbunge wa Nzega Mjini (CCM), Hussein Bashe alisema anatarajia bajeti ambayo haitaangaziwa katika kodi bali ichochee uzalishaji. Miaka karibu miwili Serikali inabana matumizi na kukusanya kodi lakini imefanya machache kuchochea uzalishaji.

“Matokeo ya hiyo hali imefanya mazingira ya biashara si mazuri na ndio maana sekta ya benki inalia kwa sababu mikopo ya asilimia iliyosilipa imefikia asilimia 12 juu ya kiwango kinachokubalika na Benki Kuu ya Tanzania asilimia 5 na hawa watu wameshindwa kulipa kwa sababu mambo hayaendi,” alisema