MNH yaweka historia uchunguzi wa ini, kongosho

Dar es Salaam. Kwa mara ya kwanza Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imeanza kufanya uchunguzi wa ini na kongosho kwa kutumia vifaa vya hadubini, yakiwa ni maandalizi ya upandikizaji wa ogani ya ini.

Huduma hiyo inafanyika Muhimbili kwa mara ya kwanza nchini na kwa nchi za Afrika Mashariki.

Akizungumza leo Juni 21 katika mkutano wa waandishi wa habari, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Mfumo wa Chakula na Ini, John Rwegasha amesema huduma hiyo ni katika hatua za kuelekea matibabu ya kibingwa ya upandikizaji ini utakaofanywa kwa kushirikiana na madaktari bingwa kutoka Hospitali ya BLK, New Delhi, India.

 

Dk Rwegasha amesema wameshirikiana na madaktari wa hospitali hiyo na wengine kutoka Afrika Kusini waliowasaidia vifaa vyenye uwezo wa kuchunguza na kutibu bila kumpasua mgonjwa.

“Hii huduma ya endoscopic (hadubibi) ni ya kwanza kabisa Afrika Mashariki, wenzetu Kenya wanafanya Agosti wakishirikiana na Wamarekani lakini sisi tumewatangulia tumeweza kuthubutu. Tayari vifaa vimeshaingia nchini na kuna wagonjwa 20 wanaosubiri  huduma,” amesema.

Dk Rwegasha amesema tangu Jumatatu walianza kutoa matibabu ya huduma za kongosho na ini kwa kutumia mfumo wa hadubini wa X Ray.

“Tumesaidia wagonjwa 25, zamani ilikuwa  lazima wakapimwe nje ya nchi, tunaushkuru uongozi wa Muhimbili kwa kusafirisha hawa watalaamu kuja kutoa ujuzi hapa,” amesema.

Mtaalamu wa magonjwa ya ini kutoka BLK India, Dk Yogesh Batra amesema utaalamu huo umelenga kuiongezea ujuzi MNH katika maeneo ambayo hayajawahi kufanyiwa kazi kwa kuleta tekolojia mpya.