Rais Magufuli aimwagia sifa TTCL

Wafanyakazi wa Shirika la Simu Tanzania (TTCL) wakifuatilia hotuba ya Rais John Magufuli wakati wa hafla ya kukabidhi gawio kwa Serikali iliyofanyika jijini Dar es Salaam jana. Picha na Anthony Siame

Dar es Salaam. Rais John Magufuli amewataka Watanzania kulitumia Shirika la Simu la TTCL kwa sababu ni lao na faida inayopatikana inarudi kwao kupitia utekelezaji miradi mbalimbali ya maendeleo.

Akizungumza wakati wa kupokea gawio la Sh1.5 bilioni kutoka TTCL jijini Dar es Salaam jana, Rais Magufuli alizitaka pia taasisi na mashirika ya Serikali kutumia huduma za TTCL na kusisitiza kuwa atashangaa kuona mashirika hayo yanatumia mitandao mingine. Alilitaka shirika hilo kubuni bidhaa mbalimbali ili kuhimili soko la ushindani na kupata fursa ya kujitanua zaidi, huku akitolea mfano wa shirika la simu la Ethiopia ambalo lilikusanya Dola 1 bilioni za Marekani mwaka 2016.

“Unapojiunga na TTCL ni kama kuweka benki hela zako,” alisema Rais Magufuli na kubainisha kwamba fedha zinazopatikana ndizo hujenga reli, barabara, kujenga shule, vituo vya afya na kutoa elimu bure.

Hata hivyo, Rais Magufuli alionyesha kushangazwa na shirika hilo kutolipa gawio kwa Serikali kwa miaka 15 lilipokuwa na ubia na kampuni ya Bhart ya India.

“Nakumbuka shirika hili lilikuwa na mkurugenzi wake, tena alikuwa dokta lakini haku-perform,” alisema Rais Magufuli. Kuhusu umiliki wa kampuni ya Airtel Tanzania, Rais Magufuli alisema mazungumzo na kampuni ya Bhart yanaendelea na kuwataka wanaohusika kutetea maslahi ya Taifa.

“Nimeambiwa TTCL imeongeza idadi ya wateja kutoka 247,000 mpaka 800,000. Hayo ni mafanikio makubwa yanaonyesha uamuzi wa Serikali kuirudisha serikalini (TTCL) ulikuwa sahihi,” alisema.

Katika hafla hiyo, Rais Magufuli alizindua pia mawasiliano kwa njia ya video (teleconferencing) na kuzungumza moja kwa moja na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliyekuwa Dodoma na Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd. “Nina uhakika siku moja Tanzania inaweza ikawa first world (nchi ya ulimwengu wa kwanza),” alisema.

Naye Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Balozi Seif alisema wakati umefika kwa taasisi za umma, binafsi na wananchi kurejesha matumaini katika huduma za mawasiliano kupitia TTCL.

Aliyasema hayo wakati wa uzinduzi wa mawasiliano kwa njia ya video yaliyofanyika mjini Unguja na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa Kassim akiwa jijini Dodoma.

Awali, meneja wa TTCL Kanda ya Zanzibar, Mohamed Yussuf Mohamed alimweleza Balozi Seif kuwa hivi sasa wanakamilisha ufungaji wa baadhi ya vifaa vitakavyowawezesha viongozi wakuu kuzungumza kwa pamoja wakiwa maeneo mbalimbali