Upande wa Machar wapinga makubaliano

Muktasari:

Naibu msemaji wa kundi hiko, Puok Both Baluang amesema makubaliano hayo ya Kampala ni kama yale ya awali mjini Addis Ababa, ambayo pia waliyakataa.

Juba, Sudan Kusini. Kundi moja la waasi nchini Sudan Kusini linalomuunga Riek Machar (pichani), limeyakataa makubaliano yaliyofikiwa mwishoni mwa wiki iliyopita ambayo yangemruhusu kurejea katika wadhifa wake wa zamani wa kuwa makamu wa rais.

Naibu msemaji wa kundi hiko, Puok Both Baluang amesema makubaliano hayo ya Kampala ni kama yale ya awali mjini Addis Ababa, ambayo pia waliyakataa.

Katika makubaliano hayo, Riek Machar atakabidhiwa tena wadhifa wa makamu wa rais, wadhifa aliouacha mwaka 2013 na kusababisha vita vya wenyewe kwa wenyewe katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki.

Hapo awali msemaji wa Machar, Lam Gabriel Paul alisema kuwa Machar alikubali makubaliano hayo na kuwa Rais Salva Kiir atabakia kuwa kiongozi mkuu wa nchi hiyo inayokumbwa na vita.

Kwa mujibu wa makubaliano hayo mapya, kutakuwa na makamu wa rais wanne, ambapo Machar atakuwa makamu wa kwanza wa rais. Makubaliano hayo yanafuatia mazungumzo yaliyofanywa mwisho wa wiki iliyopita nchini Uganda chini ya upatanishi wa Rais Yoweri Museveni.

Pande mbili hizo hasimu nchini Sudan Kusini zimehusika katika mauaji ya ulipizaji kisasi ambayo yaliibua migawanyiko ya kikabila. Makumi ya maelfu ya watu wameuawa na mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi kufuatia machafuko hayo.

Awali, Waziri wa Mambo ya Nje wa Sudan, Al Dierdiry Ahmed alisema kuwa imeafikiwa kwamba kutakuwepo makamu wanne wa rais; yaani makamu wawili wa rais waliopo hivi sasa pamoja na Riek Machar, na nafasi ya nne ya makamu wa rais atapangiwa mwanamama kutoka kambi ya upinzani.

Itakumbukwa kuwa mrengo wa upinzani nchini Sudan Kusini na serikali ya nchi hiyo wamefikia makubaliano Kampala mji mkuu wa Uganda katika juhudi za kuhitimisha vita vya ndani nchini Sudan Kusini. Vita hivyo vilianza mwaka 2013 baada ya hitilafu za kisiasa kati ya Rais Salva Kiir na aliyekuwa makamu wake, Machar kusababisha machafuko ya ndani.

Hivi karibuni waasi wa Sudan Kusini walitangaza kuwa muda zaidi unahitajika ili kufanikisha mchakato wa amani ya kudumu nchini humo na kwamba itakuwa jambo la muhimu kuvipatia ufumbuzi vyanzo vikuu vya vita vya wenyewe kwa wenyewe huko Sudan Kusini.

Waasi hao walisema hayo katika taarifa yao baada ya mazungumzo ya amani yaliyofanyika Ethiopia.

Hiyo ilikuwa mara ya kwanza viongozi hao kukutana tangu mwaka 2016 baada ya makubaliano ya amani kuvunjika na kuibuka tena mapigano kati ya vikosi vya pande mbili hizo.

Waasi wa Sudan wa SPML/SPLA (IO) wamesema kuwa ufumbuzi wa vita vya ndani vya miaka mitano nchini humo vilivyoua makumi ya maelfu ya watu na kuwalazimisha wengine zaidi ya milioni tatu kuwa wakimbizi ni kuurejelea mkataba mkuu wa amani ujulikanao kama (CPA). Mkataba huo wa amani ulifikiwa mwaka 2005 kati ya Sudan na Sudan Kusini kwa lengo la kuhitimisha vita vya ndani na kuifungulia njia Sudan Kusini kuweza kujitenga.

Hayo yanajiri wakati hivi karibuni, msemaji wa waasi, James Gatdet Dak amehukumiwa kifo baada ya kupatikana na hatia ya uhaini.