Kauli ya Rais Magufuli kuhusu wafungwa yapokewa kwa mitazamo tofauti

Muktasari:

Rais Magufuli alisema hayo juzi baada ya kumwapisha Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, Phaustine Kasike.


Dar es Salaam. Kauli ya Rais John Magufuli kwamba wafungwa wanapaswa kufanyishwa kazi usiku na mchana imepokewa kwa mitazamo tofauti.

Wakati watetezi wa haki za binadamu wakiipinga kauli hiyo, Mwenyekiti wa Bodi ya Parole, Augustine Mrema amesema inalenga kusisitiza watu wafanye kazi kwa bidii na ufanisi.

Rais Magufuli alisema hayo juzi baada ya kumwapisha Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, Phaustine Kasike.

“Anaposema wafungwa wafanye kazi usiku na mchana si kwamba alitaka wasilale, bali waongeze bidii ya kufanya kazi ili wajigharimie maana kuwahudumia kwa kuwapa chakula na matibabu ni gharama kubwa na Watanzania hawawezi kuimudu,” alisema Mrema ambaye pia ni mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Labour (TLP).

Mrema ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi alisema kauli ya Rais haina maana kwamba askari Magereza wamepewa amri ya kuanza kuwapiga wafungwa, “Haimanishi kwamba askari Magereza sasa wamepewa amri ya kupiga mateke wafungwa, Rais alilenga kueleza hataki kuona watu wazembe na goigoi.”

Hata hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga alisema ingawa Tanzania bado haijaridhia mkataba wa kimataifa unaopinga mateso kwa wafungwa, hiyo haitoi mwanya kwa mfungwa kuteswa.

“Kwa mujibu wa sheria za kimataifa, mfungwa ana haki kama walivyo binadamu wengine. Mkataba wa Umoja wa Mataifa unaelekeza mtu asiteswe hata kama yuko kizuizini,” alisema.

Mkurugenzi wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu, Onesmo Olengurumwa alisema, “Mfungwa licha ya kufungwa anakuwa na haki za binadamu za kula, kuishi na wakati mwingine anaweza kufanya shughuli akiwa gerezani za kumwingizia kipato na wakamtunzia ili siku akitoka apewe fedha za kwenda kumsaidia,” alisema.

Olengurumwa alisema, “Kauli ya kupigwa, kufanyishwa kazi usiku na mchama zinatushtua.”