Dk Bashiru awatolea uvivu wanaosaka urais Zanzibar

Wafuasi wa CCM wakimkaribisha katibu mkuu wa chama hicho, Dk Bashiru Ally katika viunga vya Ofisi Kuu ya CCM Kisiwandui mjini Unguja, Zanzibar juzi alipofanya ziara visiwani hapa. Picha na Martin Kabemba

Muktasari:

Azishukia nchi za nje akionya kuwa hawatazivumilia

Zanzibar. Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk Bashiru Ally amewatahadharisha baadhi ya wanachama wao walioanza kusaka nafasi ya urais wa Zanzibar kuwa watachukuliwa hatua za nidhamu.

Alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumza na wanachama wa chama hicho katika viwanja vya Makao Makuu ya CCM Kisiwandui mjini Unguja akiwa kwenye ziara ya kujitambulisha.

Aliwaonya kuacha mbio hizo kwa kuwa muda wa kufanya hivyo haujafika, huku akiwananga wengine kuwa hata udiwani hawauwezi.

Dk Bashiru alisema baadhi wameanza kuunda makundi na kupanga mikakati ya kuwania urais ikiwamo kufanya vikao vya siri na kubainisha kuwa, utaratibu huo ni kinyume cha katiba ya chama hicho tawala.

Alibainisha kuwa kiongozi mzuri ni yule anayeombwa kugombea si anayeonyesha uchu wa kusaka nafasi ya uongozi.

Katibu huyo mkuu alisema CCM haihitaji viongozi wa namna hiyo kwa kuwa ndiyo waliochangia kuondoa imani ya wananchi.

“Nawaomba muacheni Dk (Ali Mohamed) Shein amalize kipindi chake cha urais, msimbugudhi na makundi yenu,” alisema.

Pia, Dk Bashiru amezionya nchi mbalimbali zenye tabia ya kuingilia siasa za Tanzania.

CCM haitishwi

Dk Bashiru alisema Taifa linalobeza ushindi wa CCM uliopatikana katika chaguzi ndogo ni kuingilia siasa za nchi na kwamba, chama hicho hakitishwi na matamko ya aina hiyo. Bila kutaja taifa lolote, Dk alisema mataifa hayo yanaandika uongo na kudanganya ulimwengu kuwa Tanzania hakuna uhuru na CCM inaiba kura katika uchaguzi.

Hivi karibuni, ubalozi wa Marekani nchini ulitoa taarifa kuhusu matukio yaliyotokea wakati wa uchaguzi wa marudio wa ubunge wa Buyungu na madiwani nchini katika kata 77, ukionya baadhi ya taratibu kutozingatiwa.

Alisema chama hicho kilishinda kutokana na wananchi wengi kuwa na matumaini nacho na kwamba, CCM ni chama cha ukombozi kinapaswa kuheshimika kutokana na historia yake.

Katibu huyo alisema nchi hizo hasa zenye balozi nchini Tanzania zinatakiwa kuheshimu Katiba na miongozo ya sheria za nchi, vinginevyo watashindwa kuvumilia uchochezi unaofanywa na baadhi ya mabalozi wake.

Dk Bashiru alisema Tanzania ni Taifa huru linalojitawala na hakuna nchi yoyote itakayoweza kuyumbisha demokrasia.

Naibu katibu mkuu wa CCM Zanzibar, Abdulla Juma Saadalla alisema chama hicho kitaendelea kusimamia utekelezaji wa ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2015/2020 kwa vitendo ili wananchi waendelee kunufaika na maendeleo.