Uwekezaji kwenye kilimo cha mawese suluhisho la uagizaji mafuta ya kula

Muktasari:

Wakati tukijiandaa kwa tukio hilo la kihistoria, tunakuletea mfululizo wa makala mbalimbali zinazohusu changamoto na fursa katika sekta ya viwanda nchini, tukianza na hii ya kilimo cha chikichi na ukamuaji wa mafuta ya mawese. Endelea...

Penye miti hapana wajenzi, walisema wahenga. Msemo huu unajidhihirisha kwa Tanzania yenye kila kinachohitajika kujitosheleza na kusafirisha mafuta ya kula, lakini inaagiza bidhaa hiyo kutoka nje.

Takwimu za Chama cha Wasindikaji wa Mbegu za Alizeti (Tasupa), zinaonyesha mahitaji ya mafuta ya kula nchini ni tani 570,000 kwa mwaka lakini uzalishaji wa ndani ni tani 210,000 pekee.

Kati ya kiasi hicho kinachozalishwa nchini, tani 180,000 zinatokana na alizeti wakati vyanzo vingine vikichangia tani 30,000 zilizobaki hivyo kulilazimisha Taifa kuagiza zaidi ya tani 260,000 kila mwaka.

Tanzania huzalisha takriban tani 100,000 za alizeti kila mwaka ambazo zikikamuliwa hutoa zaidi ya tani 25,000 za mafuta ya kula huku wakulima wa pamba kutoka Kanda ya Ziwa wanaovuna tani 80,000 wakichangia tani 10,000 za mafuta baada ya kukamuliwa kwa mbegu za zao hilo.

Si alizeti na pamba pekee, kuna mbegu dahari za mafuta nchini ambazo kutokana na uwekezaji mdogo uliofanywa kwenye sekta hiyo, Tanzania itaendelea kuagiza mafuta ghafi kutoka nje hivyo kutengeneza ajira nyingi kwenye mataifa yaliyowekeza.

Kiasi kikubwa cha mafuta yanayoingizwa nchini yanatoka Malaysia ambayo hali ya hewa inafanana na Tanzania tofauti ikiwa Malaysia ni wasafirishaji wa pili wa mafuta ya kula duniani wakati Tanzania haimo kabisa kwenye orodha ya wazalishaji.

Uzalishaji

Takwimu za Benki Kuu ya Tanzania (BoT) zinaonyesha zaidi ya Sh600 bilioni hutumika kila mwaka kuagiza nakisi ya mafuta ya kula kutoka nje ya nchi.

Kiasi kikubwa cha mafuta hayo kinachozalishwa nchini kinatokana na alizeti lakini wadau wa sekta hiyo wanaamini uwekezaji wa kina ukifanywa kwenye chikichi au mawese, upungufu uliopo utabaki historia.

Mkurugenzi wa zamani wa maendeleo ya viwanda wa Shirika la Biashara, Viwanda na Kilimo (TCCIA), Adam Zuku anaamini nakisi iliyopo inaweza kumalizwa kwa kuimarisha kilimo cha chikichi kutokana na uhimilivu wa zao hilo. “Ukishapanda tu, una uhakika wa mavuno kwa miongo kadhaa. Mkulima anaweza kuvuna mara tatu mpaka nne kila mwaka. Endapo uwekezaji makini utafanywa kwenye kilimo hicho, naamini Tanzania haitaagiza mafuta ya kula kutoka nje,” anasema Zuku.

Kuvutia wawekezaji wa ndani au nje, anasema huu ni wakati muafaka wa kuhamasisha kilimo cha chikichi kwani huchukua miaka kadhaa kabla ya kuanza kupata mavuno.

Licha ya uwekezaji mpya, Zuku anasema ipo haja kuanza kuwaunganisha wakulima wadogo waliopo ili kuwaongezea uwezo. Mchakato huo anapendekeza uende sambamba na kuandaa kanzidata ya wakulima wote waliopo ili kuhamasisha kilimo hicho.

Kinachoshangaza, wawekezaji wanasema kuna uzalishaji mdogo kutosheleza uendeshaji wa viwanda vya kukamua mawese huku wakulima wakisema wanakosa soko la mavuno yao.

Msemaji wa kampuni za Bakhresa (BGC), Hussein Sufian anasema walikuwa na dhamira ya kujenga kiwanda cha kukamua mawese, lakini wana mashaka na uzalishaji wa zao hilo nchini kama utatosheleza mahitaji.

“Kuna kipindi Tanzania iliiuzia Malaysia mbegu za chikichi ambayo sasa hivi ni miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa mawese. Tanzania leo hii inaagiza kiasi kikubwa cha mafuta ghafi ya kula kutoka nchini humo. Kuna uwezekano wa Tanzania kuwa mzalishaji mkubwa wa mafuta haya endapo sera rafiki na mipango makini itawekwa,” amesema Sufian.

Anasema Tanzania inaweza kujitegemea kwa mafuta ya kula endapo uwekezaji wa kimkakati utafanywa kwenye kilimo cha chikichi na viwanda vya kusindika mawese.

Wakulima

Mmoja wa wakulima wa chikichi kutoka Kijiji cha Ugunga kilichopo wilayani Kaliua mkoani Tabora, Peter Ntendwa (62), anapinga taarifa kwamba uzalishaji wa mawese ni mdogo nchini kwa maelezo kwamba hakuna utafiti uliofanywa ukathibitisha hilo.

“Najishughulisha na kilimo hiki kwa miaka 42 hivi sasa huku nikishirikiana na wakulima wenzangu, kubadilishana uzoefu na kupeana fursa zilizopo. Kwa kipindi chote hicho, sijawahi kumuona wala kusikia kuna mtu, kampuni wala taasisi ya Serikali inafanya utafiti kuhusu sekta hii,” anasema.

Akiwa na hekta 16 za zao hilo, Ntendwa anamiliki mashine ndogo ya kukamua mawese anayoyauza kwa wateja wanaokwenda nyumbani kwake.

Kwa kila msimu wa mavuno, anasema hukamua kati ya lita 200 na 250 za mafuta hayo.

“Mpaka tunavyoongea nina zaidi ya lita 1,200 za mafuta ambayo sijui nitayauza wapi. Hakuna soko kubwa kiasi hicho,” anasema.

Kushindwa kwake kupata soko nchini, anasema kunatokana na ushindani mkubwa uliopo wa mafuta yanayoingizwa kutoka nje ambayo hupatikana nchini kote.

“Usidanganywe ndugu mwandishi, hayo ni maneno ya waagizaji wa mafuta wanaotaka kunufaika na msamaha wa kodi ili wajioongezee faida.”

Anaamini endapo kungekuwa na kiwanda kinachokamua mafuta hayo sekta hiyo ingeimarika zaidi ya maradufu na soko kubwa lingepatikana tofauti na sasa kiwango chochote wanachoweza kuzalisha kinauzwa ndani ya Wilaya ya Kaliua.

Ntendwa si peke yake anayelalamika kuhusu changamoto zinazodumaza sekta ya mafuta ya kula nchini. Godfrey Isdory ni miongoni mwa watu wa kwanza kujenga kiwanda cha kukamua mafuta hayo miaka ya 1990, lakini akakifunga kutokana na kukosa soko la uhakika.

“Yeyote anayekuambia hatuna mawese ya kutosha, anakudanganya. Nimeendesha kiwanda kwa takriban miaka 10 nikikamua zaidi ta tani tatu kila siku, lakini sikumaliza mavuno yaliyopo,” anasema.

Hata hivyo, anasema aliachana na biashara hiyo kwa sababu haikuwa inalipa kama alivyotarajia ila endapo kutakuwa na hamasa ya uwekezaji kwenye sekta hiyo, hatasita kurudi kwani anazifahamu fursa zilizopo.

Kinachohitajika kuongeza mchango wa kilimo hicho anasema ni uhamasishaji wa ujenzi wa viwanda pamoja na kuzuia uingizaji wa mafuta kutoka nje kuhakikisha kunakuwa na soko la uhakika litakalolinda viwanda vya ndani.

Kuhakikisha malighafi nyingi zaidi zinazalishwa, anasema kilimo cha mashamba makubwa ya chikichi kipewe kipaumbele sambamba na uanzishwaji wa vyama vya ushirika vitakavyowasaidia wakulima kupata mbegu za kisasa, pembejeo na ushauri wa kukabili magonjwa na changamoto nyingine zinazojitokeza pamoja na ushauri wa mbinu bora za kilimo kama inavyofanywa kwenye tumbaku.

“Mapinduzi yatatokea endapo wawekezaji wa mashamba makubwa watajitokeza na viwanda vya kukamua mawese vitajengwa. Tunahitaji uwekezaji huo ili Tanzania ijitegemee kwa mafuta ya kula,” anaeleza Isdory.

Isdory anaamini Tabora unapaswa kuweka kwenye orodha ya mikoa inayozalisha chikichi kwa kiasi kikubwa hivyo hamasa ya uwekezaji kuuhusisha pia endapo Serikali itaona ni vyema kufanya hivyo.

Kigoma ndiyo mkoa maarufu zaidi kwa kilimo hicho ikiwa na historia ya kulima chikichi na kukamua mawese tangu miaka ya 1920.

Kwa sasa, maeneo mengine yanayolima zao hilo licha ya Kigoma ni Kyela, baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Tanga na Nyasa.