Spika Ndugai aigomea Serikali bungeni, kisa watumishi wa umma

Spika wa Bunge, Job Ndugai

Muktasari:

Spika Job Ndugai ameitaka Serikali kurudia upya majibu ya swali linalohusu kupandishwa daraja kwa watumishi baada ya kutoridhishwa na majibu yaliyotolewa akisema watumishi wana maumivu

Dodoma. Spika wa Bunge, Job Ndugai ameagiza swali namba 29 la mbunge wa Lupembe (CCM), Joram Hongoli lirudiwe kujibiwa akisema halijakidhi vigezo kulingana na maumivu waliyonayo watumishi nchi.

Ndugai amesema majibu ya Serikali hayaendani na uhalisia walionao watumishi kwani haijatoa sababu za kwa nini watumishi walioajiriwa mwaka 2012 wasipandishwe madaraja yao hadi leo.

"Naitaka Serikali kuleta majibu ya kujitosheleza katika swali hili siku ya Alhamisi ijayo, watumishi hao walipaswa kupanda mwaka 2015 na 2018 lakini mnapowaacha mnadhani wataunganishwa wapi hawa," amehoji Ndugai leo bungeni Alhamisi Novemba 8, 2018

Awali, akijibu swali la Hongoli, Naibu Waziri Ofisi Rais- Tamisemi, Josephat Kandege amesema mwaka 2012/13 jumla ya watumishi 37,388 waliajiriwa na walitakiwa kupandishwa madaraja mwaka 2016/17.

"Hata hivyo, watumishi hao hawakupandishwa madaraja kutokana na utekelezaji wa kazi ya uhakiki wa watumishi hewa na vyeti vya elimu ya sekondari," amesema Kandege.

Amesema wanaendelea kuwapandisha awamu kwa awamu watumishi hao na awamu ya mwisho itakuwa katika bajeti hii ya 2018/19.