ADC wamjia juu Lissu

Mwanasheria wa CHADEMA , Tundu Lissu

Muktasari:

Kiongozi huyo wa ADC amesema kwamba chama chake kinadhani matatizo ya ndani ni vema kupambana nayo kuliko kutangazia ugomvi wako kwa mtu asiyekuhusu.

Dar es Salaam. Chama cha Alliance For Democratic Change (ADC) wameitaka Chadema itoe msimamo wake kuhusu kauli ya mwanasheria wa chama hicho, Tundu Lissu kutaka jumuiya za kimataifa zisitishe misaada kwa Tanzania.

Katibu Mkuu wa ADC, Doyo Hassan amesema kama huo hautakuwa msimamo wa Chadema ,Lissu anapaswa kuomba radhi.

Amesema kauli ya kutaka misaada isitishwe hailengi kuwatakia mema Watanzania.

"Tunadhani matatizo yetu ya ndani ni vema tukapambana nayo kuliko kutangazia ugomvi wako kwa mtu asiyekuhusu.’’

"Kwa kauli hii hizi za Chadema ni wazi wameshindwa mapambano ya ndani na sasa wanafikiria njia nyingine ambazo ni hatari zaidi katika nchi yetu,"amesema Hassan.

Amesema kama Chadema imeshindwa kupambana na CCM na Serikali yake ni wazi wawaeleze wafuasi wao kuliko kutoa matamshi ambayo yanahatarisha ustawi wa taifa letu.