AG asema Serikali inapitia upya mkataba wa Songas

Mwanasheria Mkuu wa serikali, Dk Adelardus Kilangi akizungumza bungeni alipokuwa akijibu baadhi ya hoja za wabunge waliochangia mjadala wa kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Nishati kwa mwaka wa fedha 2018/2019, jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

Ufafanuzi huo umetolewa kufuatia hoja za utata wa mkataba huo iliyotolewa na mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Jesca Kishoa.

Dodoma. Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) Dk Adelardus Kilangi amesema kuwa Serikali inafanyia mapitio upya mkataba kati yake na kampuni ya kufua umeme ya Songas ili kuhakikisha unanufaisha Taifa.

Akijibu bungeni leo Mei 25, 2018 hoja iliyotolewa na mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Jesca Kishoa aliyesema kuwa Serikali iliwekeza kiasi kikubwa katika mradi huo lakini ina hisa chache, Dk Kilangi amesema mradi huo upo chini ya utaratibu wa Ushirikiano wa Serikali na kampuni binafsi (PPP).

“Na ndani ya mkataba kuna mikataba midogo 42 kwa nature (asili) yake

ni mkataba ambao uko complex (utata). Napenda kulitaarifu Bunge mheshimiwa  mwenyekiti kuwa Serikali imechukua hatua mbalimbali,”amesema.

Amesema hatua iliyochukua ni kuitisha mikataba yote na kuifanyia rejea chini ya Sheria mpya ya Mamlaka ya Nchi kuhusiana na umiliki wa rasilimali na maliasili ya mwaka  2017.

Amesema kuwa matokeo ya marejeo hayo, yatamfanya mwanasheria mkuu wa Serikali kuishauri Serikali mambo ya kufanya.

“Tuna nafasi hata ya kurekebisha mikataba ile au terms (vipengele) za

mikataba ile, tunapewa uwezo na sheria hii mpya,”amesema.

Wakati huo huo, Naibu Waziri wa Fedha Dk Ashatu Kijaji amesema Serikali imepeleka fedha za Wakala wa Umeme Vijijini (Rea) kama zinavyokusanywa kutoka ushuru wa huduma.

Akijibu hoja za wabunge walizozitoa katika mjadala wa bajeti ya Nishati mwaka 2018/19  leo Ijumaa Mei 25, 2018 bungeni mjini Dodoma,  kuwa wizara hiyo haipeleki fedha katika miradi mbalimbali,  naibu waziri huyo amesema Sh 36 bilioni zimetolewa.

Amesema Julai, 2017 Bunge lilipitisha kukusanywa kwa Sh31.06bilioni lakini kilichokusanywa ni Sh 21.5bilioni na kwamba zilipelekwa zote kwenye mfuko wa Rea.

Amesema Agosti, 2017 walitakiwa kukusanya Sh  37.5bilioni lakini walikusanya Sh 36.7bilioni ambazo zote zilipelekwa katika mfuko huo.

“Septemba walitakiwa kukusanya Sh 36 bilioni lakini tulikusanya Sh

26bilioni. Hata hivyo tulipeleka Sh35bilioni kwasababu kulikuwa na

fedha nyingine zilitakiwa kupelekwa. Julai hadi Aprili, 2018

tumeshapeleka asilimia 99.9 ya fedha zilizotakiwa kupelekwa

Rea,”amesema.

Kuhusu hoja iliyotolewa na Mbunge wa Momba (Chadema) David Silinde kuwa ushuru wa huduma katika gesi kwenda katika mfuko mkuu wa Serikali, Dk Kijaji amesema ameomba kuletewa barua zinazodaiwa

kuandikwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania  (TRA) kwa sababu wao hawana.

“Tunachofahamu kuwa service levy (ushuru wa huduma) unakusanywa na halmashauri na hiki ndio kilichopo na ndicho kilichopitishwa katika

sheria ya fedha miaka yote na ndicho tunachokitekeleza,”amesema.