Afikishwa mahakamani kwa kuzini na mwanae

Muktasari:

Mshtakiwa ameieleza mahakama kuwa mashtaka yanayomkabili si ya kweli, kwamba ni njama za ndugu zake kutokana na kuwa na mgogoro wa ardhi

Serengeti. Mwita Charles (45) mkazi wa kijiji cha Iseresere amefikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi mfawidhi Wilaya ya Serengeti mkoani Mara kwa tuhuma za kuzini na mwanae mwenye umri wa miaka 15.

Charles amefikishwa mahakamani hapo leo Jumatano Septemba12, 2018 mbele ya hakimu wa mahakama hiyo,  Ismael Ngaile.

Mshtakiwa huyo alipoulizwa na hakimu Ngaile kuhusu uhusiano wake na binti huyo, amesema ni mwanae.

Mwendesha mashtaka wa polisi, Renatus Zakeo amesema mtuhumiwa alitenda kosa hilo Septemba 6, 2018 katika kijiji hicho kilichopo wilayani Serengeti.

Amesema kosa hilo ni kinyume na kifungu namba 158(1)(a) cha kanuni ya adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Mshitakiwa amekana shtaka hilo huku akidai ni njama za ndugu zake kutokana na mgogoro wa ardhi.

Upande wa mashtaka umesema upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na kuahirishwa hadi Septemba 26, 2018 itakapotajwa tena huku mtuhumiwa kurudishwa mahabusu.