Vigogo wengine wawili uchimbaji madini wakamatwa

Muktasari:

Wanadaiwa kufadhili uchimbaji haramu wa madini ya Tanzanite.


Mirerani. Idadi ya vigogo wa madini ya Tanzanite waliokamatwa kwa amri ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti imeongezeka na kufikia saba baada ya wengine wawili kukamatwa jana Februari 8, 2018.

Kukamatwa kwa vigogo hao kunafikisha idadi ya wachimbaji saba wa madini ya Tanzanite wa Mji Mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro na jijini Arusha wanaoshikiliwa na Polisi wakidaiwa kudhamini uchimbaji haramu wa madini hayo.

Februari 7, Mnyeti aliagiza vigogo watano wa madini hayo kukamatwa na kushikiliwa kwenye kituo cha Polisi Mirerani.

Akizungumza na Mwananchi leo Februari 9, 2018 Kamanda wa polisi mkoani Manyara, Agustino Senga amethibitisha kukamatwa vigogo hao na kushikiliwa katika kituo cha polisi Mirerani.

Kamanda Senga amesema wanawashikilia baada ya kamati iliyoundwa na mkuu wa mkoa huo kupata taarifa kuwa vigogo hao wanashiriki kuwadhamini vijana wanaoingia kwa wizi kwenye migodi ya kampuni ya TanzaniteOne yenye ubia na Serikali kwa asilimia 50 kwa 50 na Shirika la Madini la Taifa (Stamico).

Amesema bado wanaendelea na wanachunguza suala hilo na endapo uchunguzi utakamilika vigogo hao (majina yao tunayahifadhi) watafikishwa mahakamani.

"Bado tunaendelea na uchunguzi wa tukio hilo kwani watuhumiwa hao wanadaiwa kuwadhamini wachimbaji hao haramu ambao wanaingia migodini bila kibali," amesema Senga.

Amesema kuna kamati maalum iliundwa na mkuu wa mkoa huo kwa ajili ya kuchunguza suala hilo hivyo baada ya uchunguzi wa awali, ikabidi vigogo hao wakamatwe.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji Madini wa mkoa wa Manyara (Marema), Sadiki Mneney amesema wamepata taarifa za kukamatwa na kushikiliwa polisi kwa wachimbaji hao.

Mneney amesema wao kama Marema wamepanga kwenda makao makuu ya mkoa huo mjini Babati ili kuzungumza na mkuu wa mkoa huo juu ya kukamatwa kwa wachimbaji hao.

"Jumatatu ijayo tunaenda Babati kufuatilia suala hilo kwani hadi sasa hatujui ni sababu gani iliyofanya wachimbaji hao wa madini wakakamatwa na kushikiliwa na polisi," amesema.