Agizo la waziri kwa DC lamuweka ndani daktari
Muktasari:
- Hata hivyo, kosa lililomsukuma Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Dk Seif Shekalaghe kumsweka ndani daktari wa hospitali ya wilaya hiyo, Laurent Biyengo linahusiana na unywaji pombe wakati wa kazi.
Siku saba tangu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu kuwataka wakuu wa mikoa na wilaya kuacha tabia ya kuwaweka mahabusu watumishi wa umma kwa makosa ya kitaaluma, mkuu wa wilaya Maswa amemsweka mahabusu daktari.
Hata hivyo, kosa lililomsukuma Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Dk Seif Shekalaghe kumsweka ndani daktari wa hospitali ya wilaya hiyo, Laurent Biyengo linahusiana na unywaji pombe wakati wa kazi.
Septemba 25, Waziri Ummy alitoa agizo kwa wakuu hao kuacha kuwaweka mahabusu watumishi wa umma kwa makosa yanayotokana na taaluma zao.
Hata jana agizo alilitoa yeye waziri akimwagiza mkuu wa wilaya hiyo kumchukulia hatua daktari huyo kutokana na uzembe uliosababisha mjamzito kuharibikiwa na ujauzito wake akiwa hospitalini hapo.
Ummy alitoa agizo hilo kwa njia ya simu baada ya mjamzito, Salome John aliyefika hospitalini hapo kupatiwa matibabu usiku wa Septemba 27 kuharibikiwa ujauzito kwa kukosa huduma.
Waziri Ummy alitoa maelekezo hayo baada ya kupata taarifa hizo kwa njia ya ujumbe mfupi wa maandishi kutoka kwa mwandishi wa gazeti hili juu ya wagonjwa waliofika kupata huduma katika hospitali hiyo na kumkosa daktari wa zamu. “Nimemwelekeza Naibu Katibu Mkuu Tamisemi ashughulikie suala hilo,” aliandika kupitia ujumbe mfupi wa maandishi wa simu yake ya mkononi na kuutuma.
Akizungumzia tukio hilo, Mkuu wa wilaya ya Maswa, Dk Shekalaghe alisema alisikitishwa na kitendo hicho na kueleza kwamba hawezi kuwavumilia watumishi wa Serikali wa namna hiyo.
“Nimeagiza mtumishi huyo awekwe mahabusu wakati hatua nyingine za kinidhamu na kisheria zikifuata dhidi yake,” alisema.
Jeshi la Polisi katika Wilaya ya Maswa lilithibitisha kumkamata na kumuweka mahabusu daktari huyo kutokana na maagizo ya mkuu wa wilaya.
Wagonjwa waliokuwa hospitalini hapo walisema walifika kati ya saa moja hadi saa tatu usiku kwa ajili ya kupatiwa matibabu, lakini cha kushangaza daktari wa zamu hakuwepo.
Walisema licha ya wauguzi kuwepo walishindwa kuwahudumia hasa mjamzito huyo aliyekuwa akilia kutokana na maumivu aliyokuwa akiyapata kwa maelezo kuwa, taratibu haziwaruhusu hadi wanapoandikiwa cheti au maelekezo ya daktari.