VIDEO: Lugola avunja baraza la usalama barabarani

Muktasari:

Barabara mbadala kutumika kukwepa mteremko wa mlima Iwambi, Mbeya.

Mbeya. Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola amelivunja Baraza la Taifa la Usalama Barabarani na mabaraza yote ya ngazi ya mkoa.

Ametangaza uamuzi huo leo Julai 5, 2018 jijini Mbeya alipozungumza na kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa wa Mbeya na baraza la usalama barabarani mkoani humo.

Lugola amesema hajaridhishwa na utendaji wa baraza katika kukabiliana na ajali za barabarani.

"Nilikuwa namuuliza mwenyekiti wa baraza la usalama barabarani nikabaini hajui hata sheria inayoliweka baraza hilo na hata kanuni zake hazijui, hii inaonyesha hatuna baraza na kuanzia sasa kwa mamlaka niliyonayo nalivunja baraza hili na nitaliunda upya," amesema Lugola.

Amesema kutokana na ajali za barabarani, amemuagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro kutekeleza  hatua saba za kimkakati ili kukomesha ajali hizo.

Wakati huohuo, Waziri wa Uchukuzi, Ujenzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe amemuagiza katibu mkuu wa wizara hiyo kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara mbadala ya kutoka Iyunga hadi Mbalizi kuepusha ajali zinazotokea eneo la mteremko wa mlima Iwambi.

Pia, ameagiza Wakala wa Barabara nchini (Tanroads) kuhakikisha unasimamia ujenzi ukamilike ndani ya mwezi mmoja.

Kamwelwe ametoa agizo alipozungumza na wananchi wa Mji wa Mbalizi akiwa ameambatana na Lugola.

Mawaziri hao wametembelea eneo la ajali iliyosababisha vifo vya watu 20 katika mteremko wa mlima Iwambi ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais John Magufuli kwamba ajali za barabarani zidhibitiwe.

Kamwelwe ameagiza barabara ya Iyunga hadi Mbalizi yenye urefu wa kilomita sita ijengwe haraka iwezekanavyo.

“Tanroads hakikisheni ujenzi huu unasimamiwa kwa umakini ukamilike kwa muda muafaka na uanze kuanzia mwezi huu," amesema.

Lugola amesema hatakubali kuwa wa kwanza kunyooshewa kidole na Rais kwa uzembe wa watu wenye mamlaka ya kusimamia sheria na kanuni za barabarani.

Mawaziri hao leo asubuhi walikwenda Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya na Hospitali Teule ya Ifisi wilayani Mbeya kuwatembelea na kuwajulia hali majeruhi wa ajali hiyo.