Akamatwa kwa kutapeli wanafunzi Shule ya Sheria

Dar es Salaam. Mtu mmoja ambaye jina lake halikuwekwa wazi anashikiliwa na jeshi la polisi kwa tuhuma za utapeli kwa wanafunzi wa Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo(Law School of Tanzania).

Naibu mkuu wa taasisi hiyo, Dk Zakayo Lukumay amesema mtu huyo amekamatwa baada ya wanafunzi kutoa taarifa kwa uongozi wa chuo akiwa kwenye maandalizi ya kumtapeli.

"Alimpigia simu mwanafunzi akimwambia kuwa atamsaidia kumbadilishia matokeo yake baada ya kufaulu hivyo anatakiwa amtumie Sh4 milioni kwa ajili ya kufanikisha hilo,"

"Taarifa za utapeli wa aina hii tumekuwa tukizipata kwa muda mrefu tulianza kwa kijichunguza wenyewe na tukathibitisha hakuna mtu ndani ya taasisi anayehusika,"

Kutokana na hali hiyo Dk Lukumay amewataka wanafunzi kuwa makini na utapeli huo na kuzingatia kanuni za mitihani ya taasisi.

"Hakuna namna ambavyo mtu anakuwezesha kufaulu au kubadili matokeo, mwanafunzi mwenyewe ndiye una uwezo huo. Sheria inaruhusu mtu kurudia mtihani hadi pale atakapofaulu,"amesema Dk Lukumay