Aliyempa mimba dada yake miaka 30 jela

Muktasari:

  • Walikuwa wakiishi kwa babu yao aliingia chumbani kwa binti huyo na kumfanyia unyama huo

Misungwi. Mkazi wa kijiji cha Usagara wilayani hapa Mkoa wa Mwanza, Charles Abel (24) amehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kwa makosa mawili ya kubaka na kumpa mimba mwanafunzi wa darasa la saba wa Shule ya Msingi Busagara.

Hukumu hiyo ilitolewa juzi na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama ya wilaya hiyo, Erick Marley baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka. Hakimu Marley alisema ushahidi uliotolewa na mashahidi watano akiwemo mwanafunzi mwenyewe, uliotolewa mahakamani haukuacha shaka yoyote.

Mwanafunzi huyo aliiambia mahakama kwamba Juni 6 saa 1:30 usiku akiwa chumbani kwake aliingiliwa na kubakwa na kaka yake ambaye ni mtoto wa baba yake mkubwa.

“Mahakama imekubaliana na upande wa mashtaka, hakuna ubishi kuwa mwanafunzi huyo mwenye umri wa miaka 13 alibakwa na kuondolewa usichana wake, kupewa ujauzito na aliyemtaja kuwa ni kaka yake waliyekuwa wakiishi pamoja kwa babu yao,” alisema Marley.

Kabla ya kusomwa hukumu hiyo, Mahakama ilimpa nafasi mshtakiwa kujitetea ambaye aliomba kupunguziwa adhabu.

Mshtakiwa alidai kuwa hawezi kufanya mapenzi na dada yake na kwamba ametengenezewa kesi hiyo kwa kuwa walikuwa hawataki aishi hapo kwa babu yake: “Naomba Mahakama inisamehe.”

Awali, mwendesha mashtaka wa polisi, Ramsoney Salehe aliiomba mahakama kutoa adhabu kali ili liwe fundisho kwa wengine wanaokatiza masomo ya watoto wa kike kwa kuwapa mimba.

Katika hukumu yake, Marley alisema Mahakama inamhukumu mshtakiwa kwa kosa la kwanza la kumbaka kifungo miaka 30 jela na kwamba, shtaka la pili la kumpa mimba atatumikia miaka 30 jela.

Hivyo, atatumikia miaka 60 lakini kwa sababu adhabu zote zinakwenda pamoja atatumikia miaka 30.