Aliyenusurika ajali MV Bukoba kuzindua album nyimbo za injili

Muktasari:

Mtoto huyo akiwa na miaka minane aliokolewa kwenye ajali hiyo ingawa wazazi wake walifariki

Dar es Salaam. Mtoto aliyeokolewa kwenye ajali ya meli ya MV Bukoba mwaka 1996 akiwa na umri wa miaka minne, Samuel Paschal anatarajia kuachia albamu yake ya video katika uzinduzi utakaofanyika April 22, 2018 mkoani Arusha.

Samuel aliokolewa kwenye ajali hiyo lakini wazazi wake wote wawili walipoteza maisha.

Akizungumza kwa njia ya simu na MCL Digital leo Machi 24, 2018 Samuel ambaye kazi zake tayari ameziachia katika akaunti yake ya ‘Youtube’amesema uzinduzi huo utaambatana na shukrani zake kwa Mungu kwa kuweza kufikia hatua hiyo.

"Natamani kumshukuru Mungu sana kwa kunifikisha hapa na uhai nilio nao na nachoomba ni sapoti ya Watanzania wenzangu kwenye kazi hii ya kipaji niliyoamua kuifanya," amesema.

Muimbaji huyo wa muziki wa injili ambaye pia kuna nyimbo amemshirikisha Tumaini Martin au Matumaini wa Kiwewe, amesema uzinduzi wake utafanyika katika Kanisa la KKKT, Dayosisi ya Kaskazini Kati, Usharika wa Sokoni Ngulelo.

Nani anifute Machozi ndilo jina la albamu yangu iliyosheheni video kali ambazo naamini kila atakayezipata atakubali tena kukata tamaa hata kama kuna jambo gumu linalomzunguka,” amesema.

Amesema waimbaji lukuki wanatarajia kumsindikiza katika uzinduzi huo akiwamo Angel Bernard.