Aliyekuwa mgombea urais NCCR -Mageuzi ajivua uanachama

Muktasari:

NCCR imesema inaheshimu uamuzi wa Dk Kahangwa.

Dar es Salaam. Mwanachama wa NCCR- Mageuzi, Dk George Kahangwa ametangaza kujiondoa ndani ya chama hicho.

Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, Dk Kahangwa alipendekezwa na NCCR-Mageuzi kuwania urais ndani ya vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ili kupitishwa kupeperusha bendera ya umoja huo.

Dk Kahangwa ambaye ni msomi wa masuala ya elimu ametangaza uamuzi huo kupitia ukurasa wake wa kijamii wa Facebook ikiwa ni kipindi ambacho kumekuwa na wimbi la wanasiasa wa upinzani kuhamia Chama cha Mapinduzi (CCM).

“Mniwie radhi kuwataarifu hili. Sioni dalili yoyote ya mwanga katika chumba cha giza nene linaloigubika NCCR- Mageuzi. Hivyo, hiari ileile niliyoitumia kujiunga, sasa naitumia kukaa pembeni,” amesema Dk Kahangwa katika ujumbe aliouweka Facebook

MCL Digital ilipomtafuta Dk Kahangwa aliyekuwa mjumbe wa Halmashauri Kuu ya chama hicho kwa njia ya simu hakupatika.

Hata hivyo, Mkuu wa Oganaizesheni na Utawala wa NCCR-Mageuzi, Florian Mbeo amethibitisha kujiondoa kwa Dk Kahangwa.

"Ni kweli amejivua uanachama,  alikieleza chama kuhusu suala hilo na hata leo asubuhi nimezungumza naye. Uamuzi aliochukua ni wa kawaida tunauheshimu," amesema Mbeo.

Akitoa maoni kuhusu ujumbe wa Dk Kahangwa Facebook, Mathias Mbeho amesema, ‘’Mkuu kwa kweli huko ulipotea gizani. Kwa wewe ulivyo unatakiwa kumuunga mkono ili kusukuma mbele gurudumu la maendeleo katika Taifa hili. Nayaona maisha yako mapya na mazuri kwenye ulingo wa siasa. Wise decision.”

Abdul Migeyo Juma amesema, ‘’Nakupongeza kwa kufanya maamuzi Dr! Ila sababu yako siyo ya kisomi hata kidogo, unadhani mwanga unaletwa na nani? asee hapa ndio nashindwa kuelewa ukombozi wa kifikra juu ya elimu tuipatayo Watanzania, Nadhani tutafika hatua ya kutowapeleka watoto shule maana matokeo ya wasomi wetu kwenye jamii yakiwa hivi mnatutia wasiwasi juu ya kusomesha watoto!! Au elimu yetu ndio inatufanya tuwe hivi? Kipindi hiki kilikuwa si sahihi kwako kutoka NCCR hata kama ni haki yako.”