ACT Wazalendo yawasemea wakulima wa mbaazi

Muktasari:

ACT Wazalendo imetaka kuharakishwa mazungumzo kati ya Tanzania na Serikali ya India.

Dar es Salaam. Chama cha ACT Wazalendo kimesema bei ya mbaazi nchini imeporomoka kutoka Sh2,500 kwa kilo mpaka Sh200.

Kutokana na hilo, kimetaka Serikali kuwatafutia wakulima soko na kufufua mazungumzo kati yake na Serikali ya India ambayo imefunga soko la zao hilo kwa nchi ambazo hazikuwa na mkataba nazo, ikiwemo Tanzania.

Hata hivyo, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage aliwahi kukaririwa akisema Tanzania ilikuwa na mkataba na India lakini soko lake lilifungiwa kimakosa na mazungumzo yanaendelea.

India ilifikia uamuzi huo Agosti 5, 2017 baada ya kuzalisha kwa wingi mbaazi.

Katibu wa Itikadi, Mawasiliano na Uenezi wa chama hicho, Ado Shaibu amesema hayo leo Jumatano Oktoba 18, 2017 alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

Amesema wakulima nchini wanalia kutokana na kuporomoka kwa bei ya mbaazi kutoka Sh2,500 kwa kilo katika msimu uliopita mpaka wastani wa Sh200 hivi sasa.

Shaibu amesema wamezunguka kufanya utafiti wa zao hilo katika mikoa mbalimbali nchini kati ya Julai na Oktoba na kubaini kuna anguko kubwa la bei. Amesema mbaazi imeporomoka bei kwa zaidi ya asilimia 100.

Amesema wamekwenda Namtumbo ambako bei ni Sh100 kwa kilo; Nachingwea, Manyara, Lindi Mjini na Lindi Vijijini bei ni kati ya Sh150 na Sh200; Masasi ni Sh200 na Manyara, Ruangwa, Arusha na Tunduru ni kati ya Sh100 na Sh200 kwa kilo.

Shaibu amesema anguko la bei limesababisha wafanyabiashara wa ndani wa nafaka kuepuka kujihusisha na biashara ya mbaazi katika msimu huu wa mavuno kwa kuogopa kupata hasara.

Alipoulizwa kuhusu suala hilo, Waziri wa Kilimo, Charles Tizeba amesema aulizwe Waziri wa Viwanda, Mwijage kwa sababu yeye ndiye anayeshughulikia masuala ya biashara.

Waziri Mwijage alipoulizwa amesema yuko safarini kuelekea Dar es Salaam na akifika atawasiliana na wataalamu wa wizara kuhusu suala hilo.