Apandikizwa figo kwa Sh22 milioni

Muktasari:

  • Mgonjwa huyo atakuwa wa pili nchini kupandikizwa figo baada ya ule uliofanywa na Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa kushirikiana na Hospitali ya BLK ya nchini India.

Dodoma. Hospitali ya Benjamin Mkapa imefanikiwa kufanya upasuaji wa kwanza wa upandikizaji wa figo kwa mgonjwa mmoja kwa gharama ya Sh22 milioni.

Mgonjwa huyo atakuwa wa pili nchini kupandikizwa figo baada ya ule uliofanywa na Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa kushirikiana na Hospitali ya BLK ya nchini India.

Akizungumza mjini hapa jana, kaimu mkurugenzi mtendaji wa hospitali hiyo, Kessy Shija alisema upasuaji huo ulifanyika kwa kushirikiana na Taasisi ya Matibabu ya Tokushukai ya nchini Japan na Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom).

Alisema upandikizaji ni endelevu na kwamba, madaktari kutoka Japan wamefika katika hospitali hiyo kuwapa ujuzi wa kuufanya.

“Sasa tumepanga mwezi wa sita (Juni) tutatoa huduma nyingine kama hii, huenda tukafanya kwa mgonjwa zaidi ya mmoja,” alisema.

Shija alisema kwamba katika mwaka mmoja watakuwa na uwezo wa kufanya upandikizaji huo kwa wagonjwa kati ya 12 hadi 20.

Makamu mkuu wa Udom, Profesa Egid Mubofu alitoa wito kwa Serikali kuharakisha sheria ya nchi na kutoa mwongozo ambao utazuia kuwepo kwa biashara ya uuzaji wa figo kama inavyofanyika nchi za Bara la Asia.

“Katika kudhibiti hili suala inabidi kuwepo na utaratibu ulio wazi kwa Watanzania pindi tutakapoanza kupandikiza figo kwa ndugu wasio na uhusiano wa karibu kuweza kujitolea baadhi ya viungo vyao kutumika pindi kifo kinapowakuta,”alisema.

Alisema upandikizaji huo umegharimu Sh 22 milioni na hivyo kuokoa zaidi ya Sh55 milioni kama ungefanyiwa nje ya nchi.

Naye mkurugenzi mtendaji wa Hospitali ya Shonan Kamakura ya Japan, Dk Shuzo Kobayashi aliahidi kuendelea kujenga uwezo kwa wataalamu wa hospitali hiyo.