Asiyeona apanda Mlima Kilimanjaro

Muktasari:

Akizungumza baada ya kushuka mlimani jana, Berlin alisema alilenga kuionyesha dunia kuwa watu wenye ulemavu wa kuona wanaweza kufanya mambo makubwa na hata kuwasaidia wanaojiweza.

Moshi. Raia wa Marekani, Dan Berlin ambaye ni mlemavu wa macho amepanda Mlima Kilimanjaro kwa lengo la kuchangisha Euro 25,000 (zaidi ya Sh50 milioni) kwa ajili ya upanuzi wa jengo la chuo cha ufundi wa magari kilichopo Himo wilayani hapa, Mkoa wa Kilimanjaro.

Akizungumza baada ya kushuka mlimani jana, Berlin alisema alilenga kuionyesha dunia kuwa watu wenye ulemavu wa kuona wanaweza kufanya mambo makubwa na hata kuwasaidia wanaojiweza.

Berlin aliyetumia muda wa siku tatu kupanda mlima huo alisema: “Nimeamua kupanda Mlima Kilimanjaro ili kupata fedha kwa ajili ya kupanua jengo la chuo cha makanika (ufundi wa magari) ambacho kitakuwa kinasomesha watoto waliokosa elimu ya sekondari na kuamua kuwa mafundi.”