Askari mstaafu JWTZ ajinyonga kwa shuka hadi kufa
Muktasari:
Askari mstaafu wa JWTZ ametumia shuka kujinyonga na mwili wake umekutwa kwenye chumba chake cha kulala usiku wa kuamkia leo.
Ngara. Askari mstaafu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Eliasi Kazoya (68) mkazi wa kijiji cha Mukibogoye wilayani hapa amejinyonga kwa kutumia kipande cha shuka.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Mukibogoye wilayani Ngara Poncian Duguza amesema askari huyo amejinyonga usiku wa kuamkia leo Septemba 14 na kwamba alijininginiza juu ya paa katika chumba chake cha kulala.
Duguza pamoja na ndugu jamaa na marafiki za mwanajeshi huyo wamesema Kazoya aliugua kwa muda mrefu maradhi ya Kifua Kikuu.
“Nimepata taarifa za mwanajeshi mstaafu huyu kujinyonga baada ya wanafamilia kufika nyumbani kwangu kunijulisha majira ya saa 12 asubuhi na mimi nikawafahamisha polisi,” amesema Duguza.
Akizungumzia tukio hilo, mke wa Marehemu Julitha Elias amesema pia mume wake aliwahi kusema kuwa atajiua.
“Kabla ya kujiua Septemba 13 alimtuma mwanaye wa darasa la saba kwenda kumnunulia wembe ambao aliutumia kukata kipande cha shuka,” amesema na kuongeza:
“Niliishi naye akiwa na maradhi haya ya kifua kikuu na alipokuwa akienda Hospitali kupewa dawa alipuuzia kumaliza dozi na ameniacha mjamzito na nina watoto wengine saba,” amesema Julieth.
Mkuu wa Kituo cha Polisi Kabanga (OCS), Benard Masakia ameshauri wananchi kutojichukulia sheria mkononi bali wawashirikishe ndugu , jamaa na marafiki kutafuta suluhisho.