Askofu Malasusa ataka lugha ya alama kufundishwa shuleni

Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Dk Alex Malasusa.

Muktasari:

  • Lugha za alama ambazo zimekuwa zikitumika kwa watu wenye ulemavu wa kusikia, zinaelezwa kutoendana na mazingira jambo linalomfanya Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Nchini (KKKT) Dayosisi ya Mashariki na Pwani Dk Alex Malasusa kutaka Serikali kuandaa mtalaa wa kuifanya lugha hiyo ifundishwe shuleni

Dodoma. Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Dk Alex Malasusa amesema lugha za alama (LAT) zinazotumika haziendani na mazingira halisi ya Tanzania na kusababisha wasiosikia kutokuelewana.

Akizungumza  leo Septemba 28, 2018 kwenye mkutano mkuu wa Chama cha Viziwi Tanzania (Chavita) na Askofu Msaidizi Chediel Lwiza, Malasusa amesema changamoto hiyo ipo hata katika shule zinazofundisha wanafunzi viziwi.

Amesema jambo hilo linasababisha wanafunzi wengi kufeli mitihani yao ya mwisho kama ilivyotokea kwenye mitihani ya Taifa ya kidato cha nne mwaka 2017.

Amesema ili kuifanya lugha hiyo ieleweke na watu wengi ni lazima Serikali itengeneze mtalaa wa lugha hiyo na kuifundisha kama somo katika shule zote nchini na vyuo.

Mwenyekiti wa Chavita, Nidrosy Mlawa amesema changamoto ya

lugha ya alama ina athari kubwa katika elimu ya viziwi, hali ambayo

inasababisha waendelee kuishi katika hali ya umaskini wa

kupindukia na kushindwa  kushiriki katika fursa mbalimbali za

maendeleo.

Amesema lugha ya alama  bado ni changa inayohitaji kuendelezwa ili

kufikia hatua ya kukidhi haja zote za mawasiliano katika jamii na hasa

katika elimu.

“Ingawa lugha ya alama ya Tanzania imefikia kukubalika rasmi kama

lugha ya kufundishia na kujifunzia kwa wanafunzi viziwi, bado

haijaingizwa kwenye mitalaa ili kufundishwa kama somo au kozi shuleni na vyuoni,” amesema.