VIDEO: Atumia saa tatu kuepusha faini kwa magari 178

Tajmohamed Abbas


Dar es Salaam. Umewahi kukamatwa na askari wa usalama barabarani na kutozwa faini kwa kosa unaloamini hukukusudia kulifanya?

Lazima ulisononeka na kutokomea au kwa wachache walipambana bila mafanikio kuzuiwa wasilipishwe Sh30,000 za faini.

Lakini ni wachache wanaweza kufikiria jinsi ya kuwasaidia madereva wengine wasitumbukie kwenye kosa kama hilo. Na wachache wanaweza kuchukua hatua kukomesha askari wanaotegea madereva wakosee badala ya kuwaelimisha.

Pengine hayo ndiyo yalikuwa kichwani mwa Tajmohamed Abbas, mkazi wa jijini Dar es Salaam, aliyeamua kuacha shughuli zake na kutumia muda mwingi kufanya kazi ya ‘utrafiki’.

Julai 16, Abbas alikumbana na mkasa kama huo, lakini hakukubali wengine wafanye kosa kama lake na kuamua kutoa elimu kwa madereva 178 katika kipindi cha saa tatu, akiwazuia wasirudie kosa lake.

Alifanyaje? Katika mahojiano na Mwananchi, Abbas alisimulia tukio zima lilivyotokea hadi akachukua uamuzi wa kusimama nyuma kidogo ya eneo alilokamatwa, akisimamisha magari na kuwaelimisha madereva wenzake wasipite eneo walilozoea kwa kuwa tayari njia imebadilishwa na wakipita wangekutana na trafiki na hivyo kutozwa faini.

“Kuna haja ya Jeshi la Polisi kutokutumia adhabu kwa kila anayekosea,” alisema Abbas.

“Makosa mengine yanaepukika kwa kutoa elimu.”

Kikosi cha usalama barabarani kingeweza kuvuna Sh5.34 milioni za faini kwa muda huo wa saa tatu katika eneo moja tu la jijini Dar es Salaam.

Siku hiyo, Abbas alikuwa akitokea katikati ya mji kwenda Mnazi Mmoja majira ya saa 9:00. alasiri. Alipofika eneo la taa za barabarani za Akiba karibu na soko la Kisutu alisimama kusubiri taa zimruhusu.

Hata hivyo, alisema taa hazikuwaruhusu na akadhani zimeharibika hivyo akakata kuelekea upande wa kulia.

“Zamani hakukuwa na makutano, ulikuwa unanyoosha moja kwa moja. Lakini hivi karibuni waliweka makutano. Mimi nimewahi kupita pale mara mbili hivi,” alisema Abbas.

Alisema mbele kidogo walisimamishwa na trafiki aliyewaeleza kuwa wamepita eneo ambalo limezuiwa. Kwa kuwa hakuwa anafahamu, ulizuka mvutano aliosema ulichukua saa moja kuanzia saa 9:30.

“Mimi nikadhani labda kibinadamu na nimevaa miwani sikukiona kile kibao. Nilimtaka askari aniandikie faini na kumuomba akanionyeshe hicho kibao,” alisema.

“Nilitegemea kingekuwa karibu, lakini tulitembea kama mita 200.Nilimwambia sikufanya uzembe, lakini askari akaniambia ni mzembe. Nikamuuliza askari kwa nini hiki (kibao cha alama ya) cha U Turn kipo hapa karibu na kile cha kuzuia kukunja kulia kiko mbali, akawa hana jibu.”

Alisema waliuliza sababu za kutotoa elimu kwa madereva wakati wanawaona wanakosea badala ya kuwatoza faini, lakini askari hawakuwa na majibu.

“Niliwaomba nijitolee kuwaelimisha watu. Nikakaa pale katika makutano, tangu saa 10:30 jioni hadi saa 1:30 usiku. Nimehesabu kwa akili yangu na mashahidi waliokuwa pale gari 178,” alisema

“Saa tatu ni sawa na dakika 180. Sasa ukichukua 180 ukagawa kwa 178 ni sawa na gari moja kwa kila dakika. Kweli gari moja kila dakika inawezekana wote kuwa ni wazembe?

“Tukichukua saa 12 unazidisha mara 60 ni 7,200 kwa siku, ukichukulia kwa mwezi 21,600 na ukizidisha mara Sh30,000 ni sawa na Sh648 milioni na hii ni kwa mwezi.”

Alisema kwa mwaka ni Sh7.8 bilioni ambazo zimeingia bila mtu kuridhika. “Tutafika kwa stahili hii?” alihoji.

Waandishi wa Mwananchi waliofika kupiga picha eneo ambalo Abbas analizungumzia, walikutana na trafiki ambaye aliwaita kuwahoji sababu za kuchukua picha. Baada ya kuelezwa mkasa wa Abbas mmoja alisema: “Hakuna kosa lolote kibao kuwa hapo kwa kuwa kipo mwanzo wa makutano. Kama kingekuwa nje ya makutano, ingekuwa sawa.

“Kibao kinaweza kukaa hata mita 500 ikiwa kilipo ni mwanzo wa makutano na kinapokwenda kuishia ni makutano, sema wanaolalamika wanakuwa kama hawajui alama za barabarani,” alisema.