Mfumuko wa bei washuka Zanzibar

Muktasari:

Umeshuka kutoka asilimia 5.9 Desemba 2017, hadi asilimia 5.2 Januari, 2018.

 


Zanzibar. Mfumuko wa bei za bidhaa mbalimbali visiwani Zanzibar umeshuka kutoka asilimia 5.9 Desemba mwaka jana hadi asilimia 5.2, Januari 2018.

Akizungumza leo Januari 7, 2018 Mkuu wa Kitengo cha Takwimu Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Zanzibar, Khamis Msham amesema baadhi ya bidhaa zilizosababisha zilizoshuka bei ni unga wa sembe, sukari, saruji, ndizi mbivu na mbichi.

“Unga wa sembe umeshuka kwa asilimia 10.2, nazi zimeshuka asilimia 18.8, ndizi mbichi zimeshuka kwa asilimia 15.6. Sukari imeshuka kwa asilimia 3.2, Saruji imeshuka asilimia 7.5, mihogo asilimia 8.1, samaki wameshuka kwa asilimia 2.3 pamoja na ndizi mbivu kwa asilimia 6.8,” amesema Msham.

Amesema bidhaa zisizokuwa za vilevi zimepungua kutoka asilimia 6.2 Desemba, 2017 hadi asilimia 1.8, mwaka 2018.

Amebainisha kuwa licha ya kushuka kwa bei hizo, kuna baadhi ya bidhaa zimepanda bei kama mafuta ya taa, dizeli na petroli.

Mhadhiri Kitengo cha Uchumi Chuo Kikuu cha Zanzibar (Suza), Suleiman Msaraka amesema kushuka kwa mfumuko wa bei za bidhaa Januari 2018 kunatokana na ununuzi wa bidhaa mbalimbali kushuka kwa kiwango kikubwa ikilinganisha na mwisho wa mwaka jana.