Babu amimina risasi ukumbini aua 50, ajeruhi zaidi ya 400

Muktasari:

 

  • Rais wa Marekani Donald Trump ametuma salamu za rambirambi kwa jamaa, ndugu na marafiki wa watu waliopoteza maisha.

Zaidi ya watu 50 wameuawa huku takriban watu 400 wakijeruhiwa katika tukio la mtu mmoja kufyatua risasi kwenye tamasha mjini Las Vegas.

Rais wa Marekani Donald Trump ametuma salamu za rambirambi kwa jamaa, ndugu na marafiki wa watu waliopoteza maisha na kusema shambulizi hilo lilikuwa baya zaidi katika historia ya nchi hiyo.

“Natoa pole nyingi kwa ndugu na jamaa waliofiwa kutokana na makasa huu hatari,” alisema Katibu wa Habari wa Ikulu, Sarah Sanders.

Sanders alisema Trump alitarajiwa kuhutubia taifa kuhusu mkasa huo baadaye. Ikulu imesema waliojeruhiwa wamefika 400.

Taarifa za polisi na mashuhuda zinasema mwanamume aitwaye Stephen Paddock, 64, akiwa amejihami kwa bunduki alifyatua risasi kutoka ghorofa ya 32 ya hoteli ya Mandalay Bay akielekeza mtutu kwenye ukumbi wa wazi wa Jason Aldean lilikokuwa likifanyika tamasha Jumapili usiku kuamkia Jumatatu. Ndani ya ukumbi kulikuwa na watu 22,000.

Baadaye naye alipigwa risasi na maofisa wa polisi katika hoteli hiyo ambako ilikutwa idadi kadhaa ya silaha. Shambulio hilo linatajwa kuwa baya zaidi katika historia ya hivi karibuni nchini Marekani.

Mkuu wa jeshi la Polisi mjini Las Vegas, Joseph Lombardo amesema shambulio hilo lilifanywa na mtu mmoja. Aliongeza kuwa polisi walikuwa na uhakika juu ya mwanamke mmoja waliyemshuku, mapema akiitwa Marilou Danley, kwamba alikuwa amebeba silaha kabla ya shambulio kufanyika lakini aliachiwa baadaye.

Mamia ya watu waliokuwa katika tamasha hilo, walianza kutoroka na kukanyagana baada ya kuanza kusikia milio ya risasi huku wakionesha nyuso za wasiwasi na huzuni.

Hadi jana asubuhi maduka yalibaki yamefungwa katika mji huo huku polisi wakiendelea na uchunguzi kubaini iwapo kuwa watu wengine walioshiriki katika tukio hili.

Ofisa huyo alisema mshambuliaji aliyekuwa amesimama katika ghorofa ya 32 ya hoteli hiyo naye aliuawa.

Lombardo alisema hakuwa katika nafasi ya kutoa maelezo ya watu waliokufa na waliojeruhiwa, lakini alithibitisha kwamba maofisa wawili wa polisi ambao walikuwa zamu ni miongoni mwa waliouawa.

“Tunaweza kusema kuwa watu 50 wamepoteza maisha na zaidi ya 200 kujeruhiwa,” alisema Lombardo. “Hili ni tukio ambalo hatujawahi kushuhudia,” aliongeza.

Msemaji wa hospitali moja jirani ambako majeruhi walipelekwa kwa matibabu amesema watu 14 kati ya waliojeruhiwa hali zao ni mbaya.

Mashuhuda wamesema mshambuliaji alirusha risasi nyingi sana na kwa mlio wa bunduki mfululizo inaonekana alitumia bunduki inayopiga mfululizo. Mamia ya watu walikimbia eneo hilo kujiokoa.

Usafiri wa ndege ulisitishwa kutoka uwanja wa ndege wa McCarran mjini Las Vegas

Asasi ya kiraia inayorekodi matukio ya uhalifu kwa kutumia mtutu wa bunduki iitwayo Gun Violence Archieve imesema shambulio hilo ndiyo baya zaidi katika historia ya Marekani tangu mwaka 1949.

Kwa mwaka 2017 pekee asasi hiyo imerekodi matukio 273 ya kushambulia watu. Asasi hiyo pia imerekodi vifo vya watu 11,621 wanaohusiana na matukio ya mashambuliao na wengine 23,433 waliojeruhiwa katika kipindi hicho.

Tukio la Mandalay Bay limekuja wiki chache tangu Spencer Hight alipofanya shambulio katika mkusanyiko nyumbani kwa mke aliyetengana naye huko Plano, Texas. Aliua watu wanane na yeye aliuawa na polisi.