Balozi wa Japan ataka mabadiliko ya Serikali yasiathiri uwekezaji

Balozi wa Japan nchini, Masaharu Yoshida akizungumza wakati wa mahojiano maalumu na waandishi wa habari wa Mwananchi, yaliyofanyika ofsini kwake, jijini Dar es Salaam. Picha na Ericky Boniphace

Muktasari:

  • Amesema kama kuna ulazima wa kufanya mabadiliko hayo, basi yafanyike kwa namna moja itakayodumu muda mrefu na kwa kufuata hatua kwa hatua ili kutoathiri uwekezaji wa muda mrefu.

Dar es Salaam. Balozi wa Japan nchini, Masaharu Yoshida ameishauri Tanzania kuwa na mfumo makini wakati Serikali nyingine inapoingia madarakani kwa sababu mabadiliko ya mfumo yanaathiri uwekezaji wa muda mrefu.

Amesema kama kuna ulazima wa kufanya mabadiliko hayo, basi yafanyike kwa namna moja itakayodumu muda mrefu na kwa kufuata hatua kwa hatua ili kutoathiri uwekezaji wa muda mrefu.

Akizungumza ofsini kwake katika mahojiano maalumu na gazeti hili hivi karibuni, Yoshida alisema Serikali ya Rais John Magufuli inafanya vizuri katika kukabiliana na rushwa, kuongeza mapato ya kodi na kupunguza matumizi yasiyo ya lazima.

Balozi huyo ameshauri kuwe na mfumo mmoja utakaodumu kwa muda mrefu zaidi na siyo kubadilishwa kila unapoingia utawala mwingine, jambo linalosababisha wawekezaji kupoteza dira.

“Haya ni masuala ya ndani lakini wawekezaji nao wanaguswa katika hili. Mfumo unaweza kubadilika lakini lazima ufanyike kwa kufuata hatua muhimu kabla ya kuanzisha mfumo mwingine,” alisema Balozi Yoshida.

Kuhamia Dodoma

Kuhusu kuhamia Dodoma, Yoshida alisema ubalozi wa Japan uko tayari kwenda huko ili kurahisisha mawasiliano yake na Serikali. Alisema suala hilo litachukua muda kidogo mpaka Serikali itakapokuwa tayari imehamia huko.

Aliitaka Serikali kuongeza idadi ya safari za ndege kutoka Dodoma kwenda Dar es Salaam ili wanadiplomasia waliopo Dar es Salaam waweze kwenda kirahisi wakati wowote wakihitaji kufanya hivyo.

“Ninatamani kungekuwa na safari nyingi za ndege za kwenda Dodoma tena nyakati za mchana, kwa sasa kuna safari chache tena za asubuhi. Dar es Salaam utabaki kuwa mji wa kibiashara, lazima usafiri uwe wa uhakika,” alisema.

Yoshida alisisitiza kwamba kuhamisha makao makuu ya nchi kunahitaji umakini mkubwa katika kuandaa mipango miji. Alisema Dodoma ikiandaliwa vizuri, itapunguza msongamano wa watu katika jiji la Dar es Salaam.

Alisema uhamisho huo utachukua muda mrefu na unahitaji rasilimali nyingi kwa ajili ya kujenga miundombinu bora itakayorahisisha maisha ya wakazi wa Dodoma lakini pia kupunguza msongamano wa watu katika jiji la Dar es Salaam.

“Ilichukua miaka 10 kwa Brazil kuhamisha makao makuu ya Serikali kutoka Rio de Janeiro kwenda Brasilia na mchakato huo ulifanikiwa. Hata hapa tunaambiwa mchakato ulianza muda mrefu ni kwa sababu ya maandalizi,” alisema.

Tahadhari ya majanga

Pia, Balozi huyo ambaye ana mwaka mmoja hapa nchini, alizungumzia suala la majanga na kuwataka wananchi kuwa makini na kuchukua tahadhari na kujua wafanye nini ili kujiokoa yanapotokea.

“Jambo muhimu ni wananchi kuwa na uelewa juu namna ya kujikinga na majanga. Serikali ina wajibu wa kutoa misaada ya kibinadamu kama vile kutoa mahema na maji kwa waathirika pamoja na kukarabati miundombinu iliyoharibika,” alisema balozi huyo.

Sera ya Viwanda

Kuhusu sera ya viwanda inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano tangu ilipoingia madarakani Novemba, 2015, Balozi Yoshida alisisitiza umuhimu wa uzalishaji wa bidhaa zinazozingatia viwango na ubora.

“Uzalishaji ni muhimu lakini elimu ya biashara ni jambo linalotakiwa kupewa kipaumbele na Serikali na wadau wote wanaohusika, wananchi wanatakiwa kushirikishwa moja kwa moja katika mpango huu,” alisema.

Alisema kwa kipindi cha miaka mitatu (2014 - 2017), Serikali ya Japan imeendesha programu za mafunzo kwa wataalamu wa fani mbalimbali ikiwamo gesi na madini ili kuzidia nchi za Afrika zinazotekeleza mkakati wa uchumi wa viwanda.

“Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo tumetoa nafasi kwa wataalamu wake kwenda Japan kupata mafunzo ya namna kampuni na viwanda vya Japan vinavyofanya kazi, kuna Watanzania 68 wanaopata mafunzo Japan katika sekta za gesi na mafuta.

“Unapotaka kuwa na uchumi wa viwanda ni muhimu kuwa na mipango na mikakati ya angalau miaka mitano, lakini msingi mkubwa ukiwa kwenye elimu,” alisema Yoshida.

Japan iko katika kundi la mataifa manane yaliyopiga hatua katika maendeleo kupitia uwekezaji wa sekta ya viwanda na imekuwa ikitegemea malighafi zinazozalishwa hapa nchini kama pamba, kahawa na madini kwa ajili ya viwanda vyake.

Sekta ya Utalii

Balozi Yoshida alisema kufanikiwa kwa Serikali ya Tanzania kufufua Shirika la Ndege (ATCL) kutasaidia kuimarisha shughuli za utalii ndani na nje ya nchi.

“Raia 7,000 hadi 8,000 kutoka Japan wanakuja Tanzania kila mwaka kutembelea hifadhi na mbuga za wanyama. Tuna kampuni nyingi za kuongoza watalii hapa nchini na ilikuwa vigumu kufanya shughuli za usafirishaji.

“Safari za ndege kwenda Ngorongoro na maeneo mengine ya nchi zitasaidia kampuni zetu kuimarisha shughuli za usafirishaji na kukuza uchumi,” alisema.

Septemba 29, 2016, Rais John Magufuli alizindua ndege mbili zilizonunuliwa kutoa kampuni ya Bombadier ya Canada ambazo zinatoa huduma ya usafiri wa anga katika mikoa mbalimbali nchini.