Baraza la ardhi lamnyang'anya mwekezaji ekari 389

Muktasari:

Mashamba yaliyofutiwa umiliki ni pamoja na  ekari 326 zilizokuwa zikimilikiwa na mke wa Waziri Mkuu Mstaafu,Esther Sumaye lililokuwa Wilayani Mvomero

Morogoro. Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ya Morogoro limemnyang'anya mwekezaji ekari 389 za ardhi na kuzirejesha kwa serikali ya Kijiji cha Melela kwaajili ya matumizi ya wananchi.

Akisoma uamuzi huo ,Mwenyekiti wa Baraza hilo Prosper Makwandi amesema baraza limeridhishwa na ushahidi uliowasilishwa mahakamani na wadaiwa ambao ni Halmashauri ya Kijiji Melela wilayani Mvomero.

Shauri hilo la madai namba 69 lilifunguliwa mwaka 2012 na mdai Kizota Wacha akiiilalamikia Halmashauri ya kijiji cha Melela kumpora eneo la ardhi lenye ukubwa wa ekari 504 ambazo alirithi toka kwa baba yake Wacha Rombo.

Katika utetezi wake Mdai (Wacha) ambaye alikuwa akiwakilishwa na Wakili Mariam Kapama aliliambia baraza kuwa baba yake alipewa eneo hilo na halmashauri ya Kijiji cha Melela mwaka 1992 hivyo anashangaa kuona kijiji kikitumia tena eneo hilo kwa matumizi ya wanakijiji.

Halmashauri ya Kijiji ambayo ilikuwa ikiwakilishwa na Wakili Alex Sikalumba imedai kuwa eneo alilopewa baba yake mdai lilikuwa ni ekari 50 na baadaye aliongezewa 15 na kufanya jumla ya ekari 65.

Mwenyekiti wa Baraza hilo,Makwandi amesema baada ya baraza kusikiliza utetezi wa pande zote mbili baraza liliridhia kwamba baba yake mdai (Wacha) alipewa ekari 50 awamu ya kwanza na kuongezewa ekari 15 na baadaye aliomba ekari 50 kama alivyoeleza mdai hivyo kufanya jumla ya ekari 115.

“Hivyo baada ya kuridhishwa na vielelezo vya pande zote  baraza linaelekeza kuwa mdai apewe ekari 115 ambazo alirithi toka kwa baba yake na ekari zilizobaki zitaendelea kuwa mali ya halmashauri ya kijiji cha Melela” amesema  Mwenyekiti huyo.

Uamuzi huo wa Baraza la ardhi umekuja wakati ambao Rais amebatilisha umiliki wa ekari 14,800 za mashamba ambayo wamiliki wake walishindwa kuyaendeleza katika wilaya za Mvomero,Kilosa na Kilombero.

Hata hivyo kwa mujibu wa Kamishna Msaidizi wa Ardhi Kanda ya Mashariki Juliana Pilla orodha ya mashambapori yaliyowasilishwa Wizara ya Ardhi kuomba kufutiwa umiliki ni zaidi ya ekari 47,000.