Monday, December 26, 2016

Bei za vyakula zalalamikiwa

 

By Pamela Chilongola, Mwananchi pchilongola@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Sikukuu ya Krismasi iliyofanyika jana, imeondoka na malalamiko kutoka kwa baadhi ya wakazi wa Dar es Salaam kutokana na kupanda kwa baadhi ya bidhaa, hususan vyakula.

Miongoni mwa vyakula vilivyolalamikiwa ni nyama iliyouzwa katika maeneo mengi Sh9,000 kwa kilo moja huku mkungu wa ndizi za kupika ukiuzwa kwa Sh60,000.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakazi wa Kigogo walisema kabla ya sikukuu kilo ya nyama ilikuwa inauzwa kwa Sh7000.

Sakina Peter alisema kutokana na kupanda kwa nyama alilazimika kununua nusu kilo.

“Bei ya kununua kilo moja imenishinda ndiyo maana nikaamua kununua hiyo nusu niwapikie wanangu,” alisema.

Abubakar Abraham anayeishi Mabibo alisema katika Soko la Buguruni mkungu wa ndizi ulikuwa unauzwa kwa Sh60,000 badala ya Sh40,000.

“Ndizi zimepanda tangu juzi na hii inasababishwa na Sikukuu ya Krismasi,” alisema Abraham.

Mfanyabiashara wa Soko la Ndizi Mabibo, Alex Silivian alisema wafanyabiashara na wakulima wanaopeleka ndizi wamepungua na kusababisha chache zinazopatikana ziuzwe kwa bei ya juu.

-->