Bili kubwa ya samaki, nyama yafanya wateja waite polisi

Muktasari:

Wakiwa wamepewa glasi za maji pekee kusindikiza mlo huo wa kawaida, watu hao walishikwa na butwaa baada ya kupewa bili ya Euro 1,145 Ijumaa.

Dar es Salaam. Watalii kutoka Japan ambao walikuwa wakipata chakula cha jioni katika hoteli moja mjini Venice, walipiga simu kuita polisi wakidai walitakiwa kulipa bili ya pauni 1.009 za Kiingereza (sawa na zaidi ya Sh6 milioni za Tanzania) kutokana na kula chakula cha kawaida.

Watu hao ambao ni wanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha Bologna, walisema waliagiza mapande matatu ya nyama na samaki wa kukaanga katika mgahawa wa Osteria da Luca ulio karibu na bustani ya St Mark's Square, kwa mujibu wa tovuti ya Daily Mail.

Wakiwa wamepewa glasi za maji pekee kusindikiza mlo huo wa kawaida, watu hao walishikwa na butwaa baada ya kupewa bili ya Euro 1,145 Ijumaa.

Marco Gasparinetti, kiongozi wa kundi la kupigania haki la April 25, alisema wanafunzi hao waliwasilisha malalamiko yao rasmi mara tu walipowasili kwenye mgahawa huo.

Wateja wengine waliopitia mgahawa huo walisema walitozwa Euro 8 kwa kila gramu 100 ya chakula cha baharini.

Kesi hiyo, ambayo Gasparinetti alisema ni tatizo jingine kwa watalii - ni kubwa kiasi cha kumlazimu meya wa jiji kuzungumzia.

Meya huyo, Luigi Brugnaro aliandika katika akaunti yake ya Twitter akisema atajaribu kuthibitisha suala hilo kutoka kwa wateja hao.

"Kama tukio hilo la aibu lilikithibitishwa, tutafanya kila tuwezalo kuwaadhibu waliohusika. Tunataka haki wakati wote," alisema.