Binti alivyokatisha masomo na kuolewa na mwalimu

Muktasari:

Mwalimu Michael Ikila anayetuhumiwa kumuoa mwanafunzi huyo mwenye miaka 17, akizungumza na juzi mbele ya mratibu elimu kata ya Nyakasungwa, Mihigo Mazima alikiri kuishi na binti huyo.

Buchosa. Mwalimu wa Shule ya Sekondari Nyakasungwa wilayani Sengerema anatuhumiwa kumuoa mwanafunzi hivyo kusababisha asiendelee na masomo ya kidato cha tano.

Mwalimu Michael Ikila anayetuhumiwa kumuoa mwanafunzi huyo mwenye miaka 17, akizungumza na juzi mbele ya mratibu elimu kata ya Nyakasungwa, Mihigo Mazima alikiri kuishi na binti huyo.

Ikila alisema aliamua kuishi naye baada ya familia yake kushindwa kumsomesha na kwamba ana mpango wa kumpeka shule baadaye.

Ofisa elimu sekondari Halmashauri ya Buchosa, Benjamin Siperato alisema hana taarifa za tukio hilo na kwamba amemuagiza mwalimu huyo kumpeleka binti huyo ofisini kwake kesho kutoa maelezo ya kutosha.

Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Emmanuel Kipole alisema wilaya na halmashauri huwasomesha watoto wanatoka katika familia maskini, hivyo anashangazwa na tukio hilo.

Kipole alisema ikithibitika mwalimu huyo amemuoa mwanafunzi atachuliwa hatua za kisheria.

Siri ilivyofichuka

Mwalimu Ikila alibainika kuoa mwanafunzi baada ya baadhi ya wanakijiji wa Nyakasungwa kulalamika kuwa kilichofanyika ni kinyume cha maadili ya kazi yake.

Wanakijiji hao walisema mwalimu huyo akiwa ni mlezi mwa mwanafunzi huyo anapaswa kuwajibishwa.

Mkuu wa Sekondari ya Nyakasungwa, Safari Mashimba alisema amepata taarifa kuhusu suala hilo.

Mashimba alisema mwanafunzi huyo (jina linahifadhiwa kwa sababu za kimaadili) alihitimu kidato cha nne mwaka 2016 na alipata daraja la tatu akiwa na pointi 25.

Alisema katika chaguo la pili alichaguliwa kujiunga na kidato cha tano mwaka 2017 katika shule ya sekondari iliyoko mkoani Tanga lakini hakuripoti alikopangiwa.

Mashimba alisema mwaka huu ndipo walipobaini kuwa ameolewa baada ya baadhi ya walimu shuleni hapo kuhudhuria shughuli ya familia kupokea posa.

Mama wa binti huyo (jina linahifadhiwa kwa sababu za kimaadili) alipoulizwa kuhusu suala hilo alisema walifikia uamuzi baada ya familia kukosa fedha za kumsomesha kutokana na baba yake kufariki dunia.

Alisema mwalimu huyo alimtorosha siku chache baada ya kumaliza mtihani wa kidato cha nne.

Alisema baada ya hapo alianza kutoa msaada kwa familia tangu mwaka 2017.

Alipoulizwa kuhusu kupokea mahari ya binti yake alisema baadhi ya walimu wa shule hiyo wakiongozwa na Gaudentius Lutaserwa walifika nyumbani kutoa mahari.

Lutaserwa, alipoulizwa juu ya suala hilo alisema alichaguliwa na mwalimu Ikila kwenda kushughulikia mahari lakini hakujua kama alikokwenda ni kwa aliyekuwa mwanafunzi wa shule hiyo.

Mdogo wa binti huyo anayesoma kidato cha pili Nyakasungwa alisema mwalimu huyo alianza uhusiano na dada yake tangu akiwa kidato cha tatuna waliendelea hadi alipomaliza kidato cha nne.

Alisema mwalimu huyo alipompatia nauli ya kwenda mjini Kahama kwa dada yao mkubwa na aliporejea mwalimu huyo alimtorosha na kumpeleka jijini Mwanza anakoishi.