Binti wa miaka 20 akamatwa na funguo bandia 154

Friday September 14 2018

 

By Jesse Mikofu na Johari Shani, Mwananchi [email protected]

Mwanza.  Polisi mkoani Mwanza wanaida kumkamata msichana Sonia Fanuel (20) mkazi wa Nyegezi jijini Mwanza akiwa na funguo bandia (master key) 154.

Polisi walibaini kuwa kati ya funguo hizo, 53 ni za vitasa na 101  za makufuli.

Akizungumza  leo Septemba 14, 2018  kamanda wa polisi mkoani hapa, Jonathan Shanna amesema msichana huyo alikamatwa Septemba 13 saa 1:45 jioni mtaa wa Rose kata ya Nyegezi.

Shanna alieleza kuwa Sonia alikamatwa baada ya wasichana wawili, Esther Isaack na Ruth Sumari, kukuta milango ya vyumba vyao imefunguliwa huku mtuhumiwa akiwa amejibanza ukutani.

 Amesema walipokagua mali zao ndani, walibaini Sh160,000 zimeibwa na nguo zenye thamani ya Sh200,000.

Katika tukio jingine, mkurugenzi wa kampuni ya ulinzi ya Mochrispo Ltd, Crispo Makori mkazi wa Buhongwa na mwenzake Simon Justin wamekamatwa kwa tuhuma za  kuharibu mabango ya kampuni ya Halotel yenye thamani ya Sh11 milioni.

Kamanda Shanna amesema watu hao walikamatwa Septemba 11,2018 maeneo ya Bugarika wilayani Nyamagana jijini hapa.

 Amesema watuhumiwa walikuwa wanatumia mabango hayo kutengenezea kofia kwa ajili ya kampuni hiyo ya ulinzi.

Wakati huohuo: Polisi wanamshikilia mganga wa jadi anayedaiwa kuendesha ramli chonganishi na kukutwa na nyara za Serikali kinyume cha sheria.

Mganga huyo mkazi wa Isangijo wilayani Magu, alikamatwa akiwa na kucha moja ya simba, mafuta ya simba, pembe moja ya swala, ndege watatu wa pori waliokaushwa, mikia miwili ya nymbu na miiba ya nungunungu bila kibali.

“Tukio hilo lilitokea Septemba 12,2018 saa 7:00 mchana wakati wa askari na maofisa wa wanyamapori wakiwa kwenye operesheni ya kuwasaka waganga hao,” amesema.

Katika tukio jingine, polisi wanamshikilia Abeid Abubakar (40) mkuu wa kitengo cha ulinzi kampuni ya mafuta ya Lake Oil jijini Dar s Salaam, kwa kumpiga na kumdhalilisha mfanya usafi wa kampuni hiyo jijini Mwanza wakimhoji kuhusu upotevu wa mafuta na fedha za kampuni hiyo.

Amesema tukio hilo lilitokea Septemba 12, 2018 saa 3:00 usiku Abubakar akiwa na mwenzake aliyejulikana kwa jina moja la Steven walikuwa wakimhoji kuhusu upotevu wa Sh86 milioni na wizi wa vilainishi vyenye thamani ya Sh42 milioni.

Shanna amesema mtuhumiwa Steven alifanikiwa kutoroka anatafutwa na kwamba, watuhumiwa wote watafikishwa mahakamani Septemba 17.