Polisi wakamata pikipiki tisa, bajaji moja za wizi

Muktasari:

Amesema kuwa watuhumiwa hao walikamatwa katika msako maalumu uliofanywa katika tarafa ya Ruhembe wilayani Kilosa.


Morogoro. Jeshi la polisi mkoani Morogoro limewakamata watu saba wakiwa na pikipiki tisa na bajaji moja zinazodhaniwa kuwa zimeibwa jijini Dar es Salaam.

Akizungumza leo Februari 9, 2018 kamanda wa Polisi mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Selemani Katumbala, Mashauri Mlinda, Danford Chengula, Emmanuel Dickson, Simon Gerard, Musa Mohamed na Abdallah Rashid.

Amesema kuwa watuhumiwa hao walikamatwa katika msako maalumu uliofanywa katika tarafa ya Ruhembe wilayani Kilosa.

Kamanda Matei amesema kuwa watuhumiwa walikamatwa katika matukio tofauti kuanzia kipindi cha mwishoni mwa mwaka jana hadi Januari, 2018.

Amesema kuwa msako huo ulifanikiwa baada ya kuwepo kwa taarifa za siri zilizotolewa na raia wema kuhusu pikipiki hizo ambazo zilikuwa zikimilikiwa na watuhumiwa hao ambao wanashikiliwa.

Kamanda Matei amesema kuwa thamani ya pikipiki pamoja na bajaji ni Sh30milioni na kwamba uchunguzi bado unaendelea ili kubaini mtandao mzima wa wizi wa vyombo vya moto.

Aidha, amesema kuwa watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani mara baada ya uchunguzi kukamilika.