Bodaboda afariki kwa kukanyagwa na lori la mizigo

Muktasari:

Hata hivyo, abiria aliyekuwa amembeba alisalimika katika ajali hiyo na kutoweka kusikojulikana kwa kile kilichelezwa na mashuhuda kuwa ni kiwewe.

Dar es Salaam. Kijana mwendesha pikipiki ambaye hakutambulika mara moja leo amekanyagwa na lori la mizigo na kufariki papo hapo katika eneo la Ubungo Mataa baada ya kukatisha barabara akihofia kukamatwa na askari wa Ulinzi Shirikishi.

Hata hivyo, abiria aliyekuwa amembeba alisalimika katika ajali hiyo na kutoweka kusikojulikana kwa kile kilichelezwa na mashuhuda kuwa ni kiwewe.

Dereva wa lori lililomgonga mwendesha pikipiki hiyo, Beatus Msigwa alisema aliona mwendesha pikipiki akikimbizwa kuelekea kwenye gari lake.

“Niliona mwendesha bodaboda akikimbizwa kuelekea barabarani na mimi nilikuwa kwenye mwendo kasi, sikujua kilichoendelea hadi kondakta wangu aliposema tumeua,” amesema Msigwa.

Kondakta wa lori hilo, Rashid Juma amesema aliona kupitia kioo cha pembeni watu wakianguka chini ya gari.

“Niliona mtu akichomoka chini ya uvungu wa gari nikamwambia dereva asimame. Baada ya kushuka nikaona pikipiki imekanyagwa na mtu ameshakufa, ila abiria wake alichomoka, nikamuuliza umesalimika, akasema amepona huku akikimbia,” amesema Juma.

Wakizungumzia tukio hilo baadhi ya madereva wa pikipiki walioshuhudia ajali hiyo, wamesema mwendesha bodaboda huyo alikuwa akikatisha barabara ya mabasi ya mwendokasi katika kituo cha Ubungo Maji, ghafla akaona askari wa Ulinsi Shirikishi ambao hukamata pikipiki zenye makosa, hivyo akaingia barabarani wakati magari yameruhusiwa.

“Tatizo ni hawa Ulinzi Shirikishi,” amesema Said Juma anayeendesha pikipiki katika eneo hilo na kuendelea:

“Huyo jamaa alikuwa akisubiri magari yapite maana yalisharuhusiwa, ndipo akawaona wale askari wanaokamata pikipiki, akataka kuwakimbia ndiyo akajikuta ameingia chini ya uvungu wa lori,” amesema.

Mwendesha pikipiki aliyejitambulisha kwa jina la Said Omar amewalalamikia askari hao wanaojulikana kama Ulinzi Shirikishi akisema wamekuwa chanzo cha ajali nyingi za pikipiki.

“Hawa askari ni tatizo kubwa, lakini hatuna la kuwafanya maana wanashirikiana na Polisi. Sisi tumezuiwa kwenda mjini lakini bado wanatufuata mpaka huku na ndiyo wamesababisha hiyo ajali,” amesema Omar.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Kinondoni, Christopher Fuime amesema hana taarifa ya tukio hilo.

“Kwa sasa nina taarifa ya tukio la moto, hiyo ya ajali sina,” amesema Fuime.