Boti yazama Rufiji, watatu wafariki dunia

Muktasari:

  • Watu watatu wamefariki dunia na wengine 18 wakinusurika baada ya boti waliyokuwa wakisafiria kuzama majini katika Mto Rufiji mkoani Pwani

Rufiji.  Watu watatu wamefariki dunia na wengine 18 wakinusurika baada ya boti waliyokuwa wakisafiria kuzama majini katika Mto Rufiji mkoani Pwani.

Boti hiyo ambayo usajili wake haujajulikana ni mali ya kijiji cha Nyaminywili kata ya Kipugira wilayani Rufiji.

Akizungumza leo Jumatano Septemba 19, 2018 Kamanda wa Polisi Mkoa wa kipolisi Rufiji, Onesmo Lyanga amesema ajali hiyo imetokea leo asubuhi katika kivuko cha Mto Rufiji.

Amesema boti hiyo ilikua imebeba watu 21 waliokuwa wakielekea katika mashamba yao.

"Ni kweli boti iliyozama ambayo usajili wake bado haujajulikana ilikua imebeba abiria 21 ikitokea mashambani eneo la Nyaminywili, ilikuwa ikiendeshwa na Jumanne Bumbo (20),” amesema Lyanga.

Amewataja waliofariki dunia kuwa ni Mwajumna Athumani (26) na mtoto wake Mwajuce Diola (10) pamoja na Wastara Said (24) maarufu kwa jina la Tumbo

Lyanga amebainisha kuwa baada ya kutoka ajali hiyo, baadhi ya wanakijiji waliwahi kuwaokoa waliokuwa katika boti hiyo.

Amesema miili ya marehemu ilipelekwa katika kituo cha afya cha Nyaminywili, mchana ilikabidhiwa kwa ndugu.

Amesema chanzo cha boti hiyo kuzama ni kugonga gogo jambo ambalo lilizua taharuki kwa waliopanda boti hiyo, ambao walikimbilia upande mmoja na kusababisha boti hiyo kupinduka, kisha kuwafunika.

Mkuu wa Wilaya ya Rufiji, Juma Njwayo amesema kati ya waliopoteza maisha, mmoja alikuwa mjamzito huku akibainisha kuwa boti hiyo imeshaondolewa majini.