Bustani, maeneo ya wazi kuboreshwa

Muktasari:

Majaliwa alitoa agizo hilo mjini hapa Julai 26 Mwaka huu, alipokuwa akizungumza na viongozi wa Dodoma kuhusiana zoezi la Serikali kuhamia Dodoma.

Dodoma. Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma imeanza kutekeleza maazimio ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ya kuboresha maeneo ya wazi (open space) na bustani.

Majaliwa alitoa agizo hilo mjini hapa Julai 26 Mwaka huu, alipokuwa akizungumza na viongozi wa Dodoma kuhusiana zoezi la Serikali kuhamia Dodoma.

Akizungumza jana Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Dodoma Melkior Komba alisema Manispaa imewaondoa wafanyabiashara katika eneo la Independence Square karibu na soko kuu ili kuipa benki ya ACB ambayo sasa itapanua eneo la bustani ili kuweka mandhari nzuri ya mji.

“Benki ya ACB imekubali kupanua bustani hiyo ili iwe nzuri zaidi. Sisi tuna maeneo mengi ya kufanyia biashara... Tatizo eneo lenye wateja wengi wa haraka haraka,” alisema.

Alisema kutokana na zoezi la kuhamia Dodoma wamechelewa kuwaondoa wafanyabiashara kwenye maeneo yasiyo rasmi kwa ajili ya kuupendezesha mji.

Alisema wafanyabiashara wa eneo hilo wanatakiwa kwenda kwenye masoko ya Chadulu, Tambukareli na Bonanza ambayo yako wazi.

Komba alisema mbali na bustani ya Independence Square, eneo la Mashujaa nalo linatafutiwa mtu wa kuliendeleza.

“Wamejitokeza watu watatu wawili wa Dodoma wanataka kuweka michezo ya watoto na mwingine raia wa nje ya nchi anayetaka kulitengeneza eneo hilo kuwa sehemu ya watu kupumzikia,” alisema.

Alisema hadi sasa wamejitokeza wawekezaji watano wanaotaka kuwekeza katika maeneo ya wazi lakini bado wapo katika mazungumzo. Komba alisema kuna maeneo mengine ya wazi ambayo walishakabidhiwa na Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA), lakini bado hayajapata wawekezaji.

Komba alisema wawekezaji watakapopatikana, watu waliojenga kwenye maeneo ya wazi watabomolewa kwa sababu makubaliano ni kujenga majengo ya muda mfupi.

Alisema maeneo ya wazi katika mji wa Dodoma yapo 15 ambayo mengine yapo katikati ya mji na mengine nje ya mji.

Kuhusu Nyerere Square, alisema wako katika majadiliano ya mwisho na CDA ili waweze kukabidhiwa na kulitafutia mwekezaji.