CAG akuna kichwa kusaidia watumishi waathirika wa VVU

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad

Muktasari:

Profesa Assad alitoa kauli hiyo na kuonyesha masikitiko kuhusu uamuzi wa Serikali wa kumpa Sh15.5 milioni, wakati aliomba Sh147 milioni kwa mwaka wa fedha 2016/17.

Dodoma. Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad atalazimika kutembeza bakuli ili kufikia malengo ya kuwasaidia watumishi 35 wa ofisi yake wanaoishi na virusi vya Ukimwi, baada ya Serikali kumgomea mapendekezo yake.

Profesa Assad alitoa kauli hiyo na kuonyesha masikitiko kuhusu uamuzi wa Serikali wa kumpa Sh15.5 milioni, wakati aliomba Sh147 milioni kwa mwaka wa fedha 2016/17.

Hata hivyo, Kamati ya Bunge ya Ukimwi, ilionyesha kumuunga mkono kwamba kiwango kilichopendekezwa kutolewa na Serikali kwa watumishi hao wanaoishi na VVU hakitoshi.

Akizungumza ofisini kwake Mjini Dodoma jana, Profesa Assad alisema atalazimika kutumia njia nyingine za kuomba fedha sehemu nyingine.

“Serikali imependekeza tupewe Sh15 milioni na mtu apatiwe Sh150,000 kwa mwezi, ninao watu 35 kati yao 30 wapo Dar es  Salaam na watano mikoani,” alisema.

Aliahidi kutumia njia zingine ikiwamo kuomba fedha kwa mashirika ya nje na taasisi za ndani, ili  kuwawezesha watumishi wake wasiteteleke.

Mwenyekiti wa Kamati ya Ukimwi, Husna Mwilima alisema ipo haja ya kuisemea ofisi hiyo kutokana na unyeti wake.