Thursday, September 14, 2017

CCM watishana Zanzibar

Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Zanzibar), Dk Abdalla

Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Zanzibar), Dk Abdalla Juma ‘Mabodi’ akizungumza na viongozi wapya wa ngazi za matawi hadi jimbo katika tawi la Ijitimai, Mwanakwerere. 

By Haji Mtumwa, Mwananchi

Zanzibar. Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dk Abdulla Juma 'Mabodi’ amesema hawatawavumilia wanachama na viongozi wanaotumiwa na vyama vya upinzani kuvuruga mshikamano uliopo ndani ya chama hicho.

Ametoa kauli hiyo leo Alhamisi akihitimisha ziara ya kuimarisha chama hicho na kuwapa mikakati ya kiutendaji viongozi wapya waliochaguliwa kuanzia ngazi ya matawi katika tawi la Ijitimai jimboni Mwanakwerekwe.

Amesema katika uchaguzi unaoendelea ndani ya CCM wanachama wasaliti wawekwe kando kwa kutopewa nafasi za uongozi na za kiutendaji ili kunusuru uhai wa chama hicho kisiasa.

Pia, amewaonya viongozi na wanachama wanaouza kadi za uanachama kwa wapinzani akiwataka waache tabia hiyo na atakayebainika atachukuliwa hatua za kimaadili kwa mujibu wa katiba ya chama hicho.

Amewasihi viongozi waliochaguliwa kuzitendea haki nafasi zao kwa kushuka ngazi za chini kutafuta wanachama wapya na hasa wa vyama vya upinzani ili mwaka 2020 upatikane ushindi wa kihistoria.

Mabodi amewataka viongozi hao wapya kuwatumia wanasiasa wakongwe na wazee wa chama hicho kujifunza itikadi na historia ya CCM ili watekeleze kazi zao kwa ufanisi.

Amesema CCM inaendelea kusimamia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2015/2020  ili kero zinazowakabili wananchi ziweze kutafutiwa ufumbuzi kabla ya uchaguzi mkuu ujao.

-->