CCM yaapa kutoa ushirikiano katika vita dhidi ya rushwa

Muktasari:

  • Ahadi hiyo ilitolewa juzi na Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mara, Samuel Kiboye alipokuwa akizungumza na wajumbe wa kamati ya siasa ya chama hicho na kutolea mfano alivyofanikisha kutiwa mbaroni kwa askari polisi wawili na ofisa mmoja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), mkoani humo wanaotuhumiwa kudai rushwa ya Sh10 milioni kutoka kwa mmoja wa wafanyabiashara.

Musoma. Chama cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Mara kimeahidi kushirikiana na vyombo na mamlaka husika kupambana na vitendo vya rushwa.

Ahadi hiyo ilitolewa juzi na Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mara, Samuel Kiboye alipokuwa akizungumza na wajumbe wa kamati ya siasa ya chama hicho na kutolea mfano alivyofanikisha kutiwa mbaroni kwa askari polisi wawili na ofisa mmoja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), mkoani humo wanaotuhumiwa kudai rushwa ya Sh10 milioni kutoka kwa mmoja wa wafanyabiashara.

Akifafanua zaidi, Kiboye alisema watumishi hao wa umma walitaka fedha hizo ili kumruhusu mfanyabiashara huyo (jina linahifadhiwa) kupitisha shehena ya mizigo kutoka nchi jirani bila kulipa ushuru. “Baada ya kutakiwa kutoa rushwa, mfanyabiashara huyo alinitaarifu, nikashirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kuandaa mtego uliowanasa,” alisema.

Kamanda wa Takukuru mkoani Mara, Alex Kuhanda alikiri polisi wawili na ofisa mmoja wa TRA kukamatwa Aprili 2 kwa tuhuma za kuomba rushwa na taratibu za kuwafikisha mahakamani zinakamilishwa.