CEOrt yazipa somo sekta binafsi

Mwenyekiti wa Umoja wa Maofisa Watendaji Wakuu wa Kampuni Binafsi nchini (CEOrt), Ali Mafuruki

Muktasari:

  • Mwenyekiti wa Umoja wa Maofisa Watendaji Wakuu wa Kampuni Binafsi nchini (CEOrt), Ali Mafuruki alisema hayo juzi alipozungumza na waandishi wa habari jijini hapa.
  • Alisema changamoto mbalimbali ni kikwazo katika jitihada za kukuza uchumi wa Tanzania.

Dar es Salaam. Sekta binafsi hazina budi kushirikiana kutatua changamoto zilizopo ili Tanzania ifikie malengo ya kiuchumi, imeelezwa.

Mwenyekiti wa Umoja wa Maofisa Watendaji Wakuu wa Kampuni Binafsi nchini (CEOrt), Ali Mafuruki alisema hayo juzi alipozungumza na waandishi wa habari jijini hapa.

Alisema changamoto mbalimbali ni kikwazo katika jitihada za kukuza uchumi wa Tanzania.

Alizitaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni ukosefu wa nishati ya umeme wa uhakika kwa ajili ya viwanda, kukosekana kwa miundombinu bora itakayosaidia uwekezaji na biashara na kudhibiti uharibifu wa mazingira.

Mufuruki alisisitiza matumizi ya nishati mbadala ili kuondokana na utumiaji mkaa unaosababisha kukatwa kwa zaidi ya tani 50,000 za miti kwa mwaka.

Alisema kuna haja ya kuendelea kuwapo majadiliano ya pamoja kati ya sekta binafsi na Serikali ili kuhamasisha maadili ya uongozi na kupambana na rushwa.

“Tunatambua Serikali na sekta binafsi zinaungana kwa namna fulani, moja haiwezi kufanikiwa bila nyingine. Hivyo, bila uhusiano mzuri ni wazi tutashindwa kufanya vizuri,” alisema Mufuruki.

Alisema CEOrt inajipanga kwa ajili ya ajenda zinazolenga kuhakikisha sekta binafsi inakabiliana na changamoto za kiuchumi na kusaidia nchi kufikia malengo yake ya kiuchumi.

Katika hatua nyingine, Mufuruki alisema CEOrt inaunga mkono jitihada zinazoendelea kupambana na dawa za kulevya nchini.

“Wote tunaona jinsi Tanzania ilivyochafuka kwa sababu ya dawa za kulevya jambo ambalo miaka 20 iliyopita halikuwapo kwa kasi hii. CEOrt tutafanya kila linalowezekana kuunga mkono jitihada hizi,” alisema.