CRDB yachomoza kwa usalama duniani

Muktasari:

Utafiti uliofanywa na taasisi ya kimataifa ya Global Finance ulihusisha nchi 106 na taasisi husika zikawekwa kwenye makundi ya benki 50 salama zaidi duniani na benki 50 za biashara salama zaidi duniani.

Benki ya CRDB imetajwa kuwa miongoni mwa taasisi salama zaidi za kifedha duniani, hivyo kuinawirisha Tanzania na kuifanya kuwa kati ya nchi 11 barani Afrika zilizokidhi vigezo hivyo.

Utafiti uliofanywa na taasisi ya kimataifa ya Global Finance ulihusisha nchi 106 na taasisi husika zikawekwa kwenye makundi ya benki 50 salama zaidi duniani na benki 50 za biashara salama zaidi duniani.

Makundi mengine ni benki 50 salama zaidi kutoka nchi zinazoibukia kiuchumi, benki salama zaidi za Kiislamu na benki bora kwa kanda za Afrika, Asia, Ulaya, Mashariki ya Mbali na Amerika.

Kukidhi vigezo na kuwamo kwenye orodha hiyo, benki 1,000 kubwa zaidi zilifanyiwa tathmini kwa kuzingatia vigezo tofauti.

Mkurugenzi wa idara ya habari wa Global Finance, Joseph Giarraputo alisema kulikuwa na changamoto wakati wa kukamilisha mchakato huo na hasa kwa benki zenye matawi kwenye zaidi ya nchi moja na zinahudumia wateja wenye ofisi katika mataifa tofauti.

“Licha ya juhudi tulizozifanya kuzihuisha, kanuni za uendeshaji wa benki zimekuwa tofauti kwa kila nchi kutokana na changamoto zilizopo pamoja na rasilimali,” alisema.

Mkurugenzi wa masoko, utafiti na huduma kwa wateja wa CRDB, Tully Mwambapa alisema ushirikiano wa wafanyakazi wa taasisi hiyo ndiyo chachu ya mafanikio ndani na nje ya mipaka.