CWT Tarime yampa onyo mkurugenzi

Muktasari:

Onyo hilo limetolewa na Mwenyekiti wa CWT wilayani humo, Shirikisho Nyagoseima kuhusiana na maagizo ya Mkurugenzi wa Mtendaji wa Halmashauri ya Mji wa Tarime, Elias Ntiruhungwa kuwaamrisha watumishi kukesha kwenye mkesha wa Mwenge.

Tarime. Chama cha Walimu Tanzania (CWT) wilayani Tarime, Mkoa wa Mara kimempa onyo mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo na kumtaka afuate kanuni na utaratibu wa kutoa maagizo kwa watumishi wake badala ya kutumia vitisho.

Onyo hilo limetolewa na Mwenyekiti wa CWT wilayani humo, Shirikisho Nyagoseima kuhusiana na maagizo ya Mkurugenzi wa Mtendaji wa Halmashauri ya Mji wa Tarime, Elias Ntiruhungwa kuwaamrisha watumishi kukesha kwenye mkesha wa Mwenge.

"Hatukubaliani na utaratibu huu ambao unatumia mabavu kuwalazimisha watumishi wa umma kutekeleza matakwa ya kiongozi, bali tunahitaji kupata waraka unaotaka watumishi kwenda kukesha," amesema Nyagoseima.

Mkesha wa mbio za Mwenge utafanyika Agosti 29 katika uwanja wa Chuo cha Ualimu Tarime, ambapo watumishi wa umma wameagizwa kukesha huku wakisaini mahudhurio kila baada ya saa mbili.

Agizo hilo limetolewa na Ntiruhungwa kwa kuwaita wakuu wa vitengo na vituo kuwahamasisha watumishi waliopo chini yao kulitekeleza na atakayekiuka jina lake litakabidhiwa kwa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya.

"Kwa mtumishi mwenye udhuru ataandika barua ya kuomba ruhusa na itajibiwa kulingana na sababu yake atakayokuwa ameitoa, kwa mwalimu, mkuu, msaidizi wake na wataalumu hao hawatakuwa na udhuru," amesema Ntiruhungwa.

Baadhi ya watumishi wa umma walionukuliwa wakizungumzia  suala hilo, wamesema kuamriwa kushona sare kwa fedha zao na kwenda kukesha uwanjani usiku huku wakiumwa na mbu ni jambo lisilo la busara kwa kuwa linaweza kuleta mgogoro kwenye familia.

"Hebu fikiria mwanamke mjamzito, mwenye mtoto mdogo anayenyonyesha au kuna wengine wana matatizo ya baridi leo wanaambiwa waende kulala uwanjani usiku kucha, hawajaletewa barua rasmi wala kuandaliwa mazingira rafiki hata malipo ya kuwepo kazini muda wa ziada hakuna," alinukuliwa mtumishi mmoja ambaye hakutaka kutajwa jina lake akihoji.

Makamu Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Suleiman Abdallah amehoji: “Tunahitaji kufahamu huyu mkurugenzi amepata wapi ujasiri wa kuwaamrisha walimu kwenda kukesha kwenye mkesha wa Mwenye  bila utaratibu. Kwa mtumishi atakayekwenda huko bila kupewa barua rasmi huyo hajitambui," amesema Abdallah.