Chadema yaanzisha Operesheni Ondoa Msaliti

Muktasari:

Kubenea ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo, ameeleza kuwa baada ya kukaa na viongozi wa CUF ili kujua kiini cha mgogoro huo wamebaini kuwa siyo mgogoro ndani ya chama, bali unachochewa na CCM wanaomtumia Profesa Lipumba ambaye wamemuita kama ni msaliti

Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimetangaza operesheni maalumu ijulikanayo kama Ondoa Msaliti Buguruni (OMB) kwa lengo la kutatua mgogoro unaokikabili Chama cha Wananchi (CUF).

Operesheni hiyo ya kidemokrasia imeanza rasmi leo Julai 10, ambapo vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vimelenga kumuunga mkono Katibu wa CUF, Maalim Seif.

Akizungumza leo wakati wa kutangaza operesheni hiyo, Makamu Mwenyekiti wa Chadema kanda ya Pwani, Saed Kubenea amesema kuwa mgogoro huo una athari kubwa kwa vyama vya upinzani hivyo  wameamua kuungana pamoja ili kuimarisha vyama vya upinzani chini ya mwavuli wa Ukawa.

Kubenea ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo, ameeleza kuwa baada ya kukaa na viongozi wa CUF ili kujua kiini cha mgogoro huo wamebaini kuwa siyo mgogoro ndani ya chama, bali unachochewa na CCM wanaomtumia Profesa Lipumba ambaye wamemuita kama ni msaliti. 

"Sisi kama Chadema tumeamua kuwasaidia viongozi na wanachama wa CUF kumuondoa msaliti Lipumba Buguruni na kutupa nguo zake na viongozi halali wa CUF watarudi Buguruni, "amesema Kubenea. 

 Kadhalika amesema pamoja na mambo mengine, chama kimeazimia kuwa mameya wa Manispaa zote za Jiji la Dar es Salaam wasitoe ushirikiano kwa viongozi wenye ushirikiano na Profesa Lipumba.