Chadema yataka Takukuru ichunguze wabunge wake kutimkia CCM

Aliyekuwa Mbunge Serengeti, Ryoba Chacha.

Muktasari:

  • Ryoba Chacha ni Mbunge wa Serengeti aliyetangaza kuhamia  CCM huzi usiku Septemba 27,2018 na kufanya idadi ya wabunge waliohama kutoka chama hicho na kuingia chama tawala kufikia wanne hadi sasa.

Dar es Salaam. Uamuzi wa aliyekuwa Mbunge Serengeti, Ryoba Chacha kutangaza kujiuzulu ubunge na kuhamia CCM, umekifanya chama chake cha zamani cha Chadema kuitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuchunguza kuona kama kuna aina mpya ya rushwa ya madaraka ambayo inawavuta wabunge wengi wa chama hicho kukimbilia chama tawala.

Ombi hilo lilitolewa leo na Mkurugenzi wa Itikadi, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema alipozungumza na Mwananchi baada ya Ryoba kutangaza kuhamia CCM kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Rais John Magufuli.

“Wabunge wamekuwa wakiahidiwa kupewa ubunge wao baada ya kuhamia CCM, hiyo ni aina nyingine ya rushwa, Takukuru waingilie kati suala hilo na kuchukua hatua,” alisema.

Mrema alidai suala la wabunge na madiwani wa Chadema kutimukia CCM haliwapi shida kwa sababu wanajua mazingira yalivyo sasa.

Alidai Mbunge huyo (Ryoba) amefanya kile alichokisema wakati wa mkutano wa Rais Magufuli huko Serengeti na kwamba hawashangazwi na uamuzi wake kwa sababu yeye siyo wa kwanza kuhama.