DC Jokate azindua tokomeza ziro

Muktasari:

Lengo la kampeni ya tokomeza ziro ni kuondoa wanafunzi wanaopata sifuri katika mitihani yao ya taifa ya kidato cha nne na sita

Dar es Salaam. Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Joket Mwegelo amezindua kampeni ya tokomeza ziro kwa wanafunzi wa kidato cha nne na cha sita ili wanafunzi wafaulu mitihani yao.

Akizungumza hayo leo Septemba 19, 2028 alipokuwa kwenye Shule ya Sekondari Chanzige, Jokate amesema kampeni hiyo ilizinduliwa tangu mwaka 2017 ambapo ilisaidia kuondoa ziro 455 mpaka 259.

amesema mwelekeo wa Serikali ni kuongeza ufaulu wa sekondari kwa kutumia mbinu ya wanafunzi kukaa kwenye makambi.

Amesema mwaka jana wanafunzi walikaa kambi kwa mwezi mmoja na nusu na mwaka huu wamekaa miezi mitatu lengo ni kufuta kabisa ziro kwenye wilaya hiyo.

"Ukimsaidia mtoto aweze kupata elimu unakuwa umeisaidia Tanzania nzima mfano kama mimi nimekuja hapa Kisarawe hivyo tunataka hawa wanafunzi kuanzia kidato cha nne na cha sita tufute ziro zisiwepo kabisa,” amesema Jokate.

Amesema kambi hiyo inasaidia watoto kusoma kwa makini na kuepuka vishawishi mbalimbali hivyo matumaini ya ufaulu yanakuwa makubwa.

Jokate amesema mbali na changamoto ya chakula kwenye makambi bado kuna uhitaji wa kuboresha miundombinu mbalimbali ikiwemo madarasa, vyoo na nyumba za walimu lengo ni kuwafanya wasome katika mazingira mazuri ili kuongeza ufaulu.

Amesema mahitaji ya uboreshaji wa kampeni hiyo ambayo itakuwa endelevu itagharimu kiasi cha Sh4.4 bilioni ambayo itasaidia kwenye makambi kwa ajili ya chakula na miundombinu hiyo.

Naye Ofisa Mipango wa wilaya hiyo, Patrivk Allute amesema wadau wa Kisarawe washiriki kwenye kampeni hiyo ili iweze kufanikiwa na iwe mfano wa kuigwa kwenye kampeni ya tokomeza ziro.