DC aipigia goti Serikali sakata la maji, alilia kiundwe chombo

Muktasari:

  • Lwenge amesema kulingana na hali ya tabia nchi inavyokwenda kwa sasa, kwa kuanzia kaya mojamoja inaweza kuanza kutumia mfumo huo huku akiwataka kuacha tabia ya kulalamika kuwa hakuna maji wakati mvua zinanyesha.

Wakati Mkuu wa Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro Agnes Hokororo akiililia Serikali iwawezeshe kuunda mamlaka yao ya maji, Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Gerson Lwenge amewataka wananchi wafikirie mfumo wa kuvuna maji ya mvua.

Lwenge amesema kulingana na hali ya tabia nchi inavyokwenda kwa sasa, kwa kuanzia kaya mojamoja inaweza kuanza kutumia mfumo huo huku akiwataka kuacha tabia ya kulalamika kuwa hakuna maji wakati mvua zinanyesha.

Hata hivyo, akizungumza mbele ya Waziri Lwenge aliyetembelea vyanzo vya maji vilivyopo wilayani humo ambavyo pia vimekuwa vikiwapatia maji wananchi wa nchi jirani, Hokororo aliiomba Serikali kuwawezesha kuunda mamlaka itakayosaidia kumaliza tatizo la maji kwa wananchi wa wilaya hiyo.

Hokororo alisema hayo baada ya kampuni ya Kili Water inayosambaza maji kwa sasa kushindwa kutoa huduma ipasavyo kwa wananchi.

Alisema kampuni hiyo iliundwa kutokana na hisa za wananchi na kwamba, miundombinu inayotumika ni ya mwaka 1994 ambayo mpaka sasa bado haijaboreshwa na kampuni hiyo haina uwezo.

“Jukumu la kutoa maji kwa wananchi ni la Serikali na ndiyo maana tumeomba mamlaka yetu kama wilaya ili tuweze kuhakikisha wakazi wote wanapata majisafi na salama kwa kusimamia vyanzo vya maji na kukarabati miundombinu,” alisema.

Akizungumzia suala la kuunda mamlaka, Lwenge alisema Serikali itaunda mamlaka ya kuendesha miradi mikubwa ikiwamo suala la usambazaji maji kwa wakazi na kwamba, tayari wizara imetenga Sh2.9 bilioni kwa mwaka 2017/18 kwa ajili ya maji kwa wilaya hiyo .

Alisema wilaya hiyo ina asilimia 57 ya upatikanaji wa maji ambayo ni kiasi kidogo ikilinganishwa na malengo yaliyopo ya asilimia 85.

Alisema ni lazima halmashauri iwe na mpango wa kujenga mabwawa na wanaweza wakajiwekea utaratibu kwa kila mwaka kujenga bwawa moja kwa kata. Meneja wa Kampuni ya Kili Water, Prosper Kessy alisema hawana ruzuku wanayotegemea kutoka serikalini kujiendesha na mara zote hutetegemea fedha wanazolipa wananchi.

Alisema vyanzo vya maji viko 29 lakini wingi wake hauna ufanisi kwa kuwa watalazimika kuajiri wafanyakazi wengi ili kuweza kuviendesha na kwamba, vingine viko mbali na husababisha gharama za uendeshaji kuwa kubwa.

“Vyanzo vingine vya maji viko mbali huwezi kuajiri mfanyakazi mmoja lazima utaweka wafanyakazi zaidi ya mmoja na je utawalipa nini kutokana na kutokuwa na fedha za kutosha kuviendesha,” alisema Kessy.