DC amtupa diwani wa Chadema mahabusu saa 48

Mkuu wa wilaya ya Sumbawanga, Halfan Haule 

Muktasari:

DC alichukua hatua hiyo kwa kile alichodai kwamba diwani huyo aliandika barua ya kuchonganisha waumini

Sumbawanga. Mkuu wa wilaya ya Sumbawanga, Halfan Haule ameagiza kukamatwa na kuwekwa ndani kwa saa 48 diwani wa Chadema.

Mkuu huyo wa wilaya alichukua uamuzi huo akimtuhumu diwani huyo kuandika barua yenye lengo la kuchonganisha waumini wa dini za Kikristo na Kiislamu hivyo kutishia kuhatarisha amani na utulivu uliopo.

Alitoa agizo hilo leo Juni 19, mchana katika kikao cha Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga, kilichofanyika kwenye ukumbi wa halmashauri hiyo mjini hapa.

Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa wilaya, diwani huyo aitwaye Felician Mavazi  wa kata ya Kizwite anadaiwa kupeleka barua katika moja ya kanisa Katoliki wilayani humo, iliyowachonganisha waumini wa kiislamu na kikristo.