DED: Kwa nini nilitoa machozi mbele ya wabunge?

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Gairo, Agnes Mkandya.

Muktasari:

Katika mahojiano mbele ya kamati hiyo yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Msekwa mjini Dodoma mwanzoni mwa wiki, Mkandya aliulizwa swali na Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Leah Komanya kuhusu ubadhirifu katika halmashauri yake, na wakati akijieleza alikuwa akibubujikwa na machozi.

Dar es Salaam. Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Gairo, Agnes Mkandya amesema utafunaji wa fedha za umma uliofanywa na watendaji ndiyo ulimtoa chozi wakati akihojiwa na Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (Laac).

“Ni kuwa kitu kilichonifanya (nitoke machozi) ni yale machungu ya ubadhirifu wa wakuu wa idara na baadhi ya watendaji kufanya wizi kwa kutumia carbon slip,” ameandika Mkandya kwenye ujumbe mfupi alioutuma kwa mwandishi wa Mwananchi.